Pata taarifa kuu
PAPA FRANCIS

Papa: Naomba radhi kwa vitendo vya unyanyasaji vilivyofanywa na mapadri wa kanisa Katoliki

Kwa mara ya kwanza toka uteuzi wake mwaka uliopita, kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis hii leo ameomba radhi hadharani kufuatia kashfa ya kulawiti watoto dhidi ya mapadri na maaskofu wa kanisa hilo. 

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Francis REUTERS/Luca Zennaro/Pool
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na kituo cha redio cha kanisa mjini Vatican, Papa Francis ameomba radhi kwa niaba ya kanisa kwa familia na watoto waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Papa Francis amekiri kanisa lake kufahamu matukio ya watoto kudhalilishwa na kwamba wanarekebisha makosa yaliyojitokeza na kuahidi kuwashughulikia kidini viongozi wote waliohusishwa kwenye tuhuma ya kulawiti watoto wadogo.

Hii ni kauli ya pili kutolewa na kiongozi wa kanisa hilo, ambapo miaka miwili iliyopita Papa Benedict wa kumi na sita naye aliomba radhi kutokana na kashfa ya mapadri kuwalawiti watoto wadogo nchini Canada na Marekani.

Wachambizi wa mambo ya dini na haki za binadamu wanaona kuwa kauli hii ya Papa Francis haitoshi kwani ili msamaha wake ukubalike ilipaswa awakabidhi kwenye vyombo vya sheria wale wote waliohusishwa kwenye tuhuma hizi.

Papa Francis ameahidi familia za wahanga na walioathiriwa na matukio haya, kuwa atashughulikia suala hili kwa umakini mkubwa ikiwemo kuwafuta uchungaji wale wote watakaobainika kuwa walitenda makosa haya.

Licha ya kuunda tume maalumu ya kuchunguza na itakayomshauri kuhusu hatua za kuchukua, Papa Francis amekosolewa kwa kuendelea kuwakingia kifua mapadri waliohusika.

Hivi karibuni kanisa hilo lilijikuta kwenye shinikizo kubwa baada ya ripoti ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kulaani vitendo hivyo na kulitaja moja kwa moja kanisa katoliki kwa kuwafumbia macho mapadri waliohusika na vitendo hivi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.