Pata taarifa kuu

LALIGA yalenga vilabu vyake kuzuru ukanda wa Afrika Mashariki

Na: Jason Sagini

Alvaro Abreu, mwakilishi wa LALIGA Afrika Mashariki akiwa jijini Nairobi, 17/08/2023
Alvaro Abreu, mwakilishi wa LALIGA Afrika Mashariki akiwa jijini Nairobi, 17/08/2023 © Jason Sagini
Matangazo ya kibiashara

Kampuni ya LALIGA inayosimamia ligi kuu ya soka nchini Uhispania wiki hii ilizindua rasmi msimu mpya na kudokeza mipango ya kuleta vilabu kutoka nchi hiyo kuzuru Afrika Mashariki siku zijazo.

Nairobi ni jiji la tano kutoka barani Afrika kuandaa kambi hii maarufu ‘LaLiga Camps’ ambao ni mpango wa kukuza talanta za wachezaji na makocha.

Awali kambi hizi zimekuwa zenye mafanikio katika miji ya Johannesburg, Cape Town, Durban na Cairo.  

Kitengo cha ligi kuu ya Uhispania kilitangaza ushirikiano na kampuni ya michezo ya video ya EA Sports, ambayo itashuhudia kampuni hiyo ikimiliki haki za majina ya ligi hiyo kuzalisha michezo ya video ya ligi hiyo baada ya kukamilika kwa mkataba wake na shirikisho la soka duniani FIFA. 

Miongoni mwa malengo ni kutekeleza zaidi usawa wa jinsia kwenye soka, kujenga misingi bora ya wachezaji na kuzima moto wa ubaguzi wa rangi kwenye msimu mpya. 

Mwakilishi wa LALIGA Afrika Mashariki Alvaro Abreu, amefichua mipango ya kuwa na timu za ligi kuu ya Uhispania kuzuru Afrika Mashariki ili kushiriki katika mechi za kirafiki kama sehemu ya kujitolea kwa ligi hiyo kuendeleza soka la mashinani kote barani Afrika. 

“Tuna nia kubwa ya kuendeleza mashindano ya ukanda wa Afrika Mashariki kwa wachezaji wasiozidi miaka 15 wavulana na miaka 17 kwa wasichana. Tunapanga kuongeza mataifa mengine kama Uganda, Ethiopia na Rwanda sababu ni lengo letu kuu,” alisisitiza Alvaro. 

Wadau wa mchezo wa soka, waliohudhuria mkutano kuhusu Kampuni ya LALIGA  jijini Nairobi, Agosti 17 2023
Wadau wa mchezo wa soka, waliohudhuria mkutano kuhusu Kampuni ya LALIGA jijini Nairobi, Agosti 17 2023 © Jason Sagini

Msimu uliopita, wasichana wa klabu ya Ligi Ndogo kutoka Kenya waliibuka washindi wa mashindano hayo.  

Mjumbe huyo alibaini tayari wapo kwenye mazungumzo na mchezaji mmoja kutoka Kenya ambaye hivi karibuni baada ya kukamilika kwa mazungumzo na familia yake huenda akawa mkenya wa kwanza kutoka kwenye akademia kucheza nchini Uhispania.

Hii ni kupitia ushirikiano wa klabu ya CD Leganes inayoshiriki ligi ya daraja la pili nchini Uhispania na klabu ya Rainbow nchini Kenya.  

“Ushirikiano kati ya Leganes na Rainbow FC utawafanya wakenya kupata fursa na kunufaika zaidi,” alisema rais wa Deportivo Leganes Jeff Luhnow. 

Klabu hiyo inajivunia awali kuwasajili wachezaji watatu kutoka Uganda na inalenga kusajili wengine kutoka Afrika Mashariki. Wachezaji hao ni mabeki Abdul-Aziz Kayondo kutoka Real Monarchs ya Marekani, Allan Enyou na Ibrahim Juma kutoka KCCA ya Uganda kwa mkopo.  

LALIGA pia ilithibitisha kuwa wapo kwenye mazungumzo ya kuanzisha ligi ya wanawake jijini Nairobi ambayo itaegemea zaidi masuala ya elimu na maendeleo. 

"Nadhani imekuwa kitu cha kipekee. Tumeweza kuonyesha video, picha na mikakati mpya kuhusu unachotarajia kwa msimu mpya kutokana na mfadhili wetu mpya wa taji EA Sports,” Abreu aliongezeka. 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.