Pata taarifa kuu
DRC-M23-UGANDA

Serikali ya DRC yasisitiza kuwa itasaini azimio la amani na sio mkataba wa amani na kundi la M23

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC, imeendelea kusisitiza nia yake ya kutia saini azimio la amani na waasi wa kundi la M23 na sio mkataba wa amani kama waasi hao na Serikali ya Uganda wanavyotaka. 

Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende
Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende Reuters
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari mjini Kinshasa, msemaji wa Serikali, Lambert Mende amesema nchi yake iko tayari kuona amani inafikiwa mashariki mwa nchi hiyo kati yake na kudni la waasi wa M23 na kwamba watatia saini azimio la amani na sio mkataba wa amani na kundi hilo.

Waziri Mende ameongeza kuwa wao kama Serikali hawawezi kutia saini mkataba wa amani na kundi ambalo tayari limeshatangaza kuachana na uasi mashariki mwa nchi hiyo pamoja na wapiganaji wake kujisalimisha kwa lengeo la kujumuishwa kwenye Serikali.

Waziri Mende ameishushia lawama utawala wa Kampala akihoji maslahi yao na mzozo wa DRC kwa kile Serikali ya Kinshasa inadai ni kwanini wanalazimisha utawala wao usaini mkataba wa amani na kundi la M23 na sio azimio.

Kiongozi huyo ameenda mbali zaidi na kudai kuwa kama Uganda haina maslahi na kundi la M23 wala machafuko yanayoendelea mashariki mwa DRC ni kwanini waendelee kusisitiza kutiwa saini mkataba wa amani kati yake na kundi ambalo halipo.

Kauli ya waziri Mende inakuja wakati huu ambapo utawala wa Uganda umeshatangaza wazi kuwa hautawakabidhi kwa namna yoyote ile viongozi wa kijeshi wa kundi la M23 kwa utawala wa Kinshasa mpaka pale nchi hiyo itakapotia saini mkataba wa amani.

Mara baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya amani mjini Kampala juma hili, Serikali ya Uganda kupitia kwa msemaji wake Ofwono Opondo ilieleza kusikitishwa kwake na hatua ya ujumbe wa DRC kutotokea kwenye shughuli ya utiaji saini mkataba wa amani.

Serikali ya Kinshasa inasema kuwa ni lazima azimio hilo litiwe saini hivi karibuni vinginevyo wao kama Serikali watalazimika kuchukua hatua zaidi kuwakabili waasi hao na makundi mengine ya waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.