Pata taarifa kuu
MISRI

Morsi: Mimi bado ni rais halali wa Misri, sitambui mapinduzi dhidi yangu

Rais wa Misri aliyepinduliwa madarakani na jeshi, Mohamed Morsi ameendelea kusisitiza kuwa yeye ni kiongozi wa halali wa taifa hilo na kwamba hatambui mamlaka zilizomuondoa madarakani, wakili wake amesema. 

Mohamed Morsi akiwasili mahakamani hivi karibuni wakati alipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza
Mohamed Morsi akiwasili mahakamani hivi karibuni wakati alipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza REUTERS/Egypt Interior Ministry
Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Mosri imesomwa na mawakili walioenda kumtembelea gerezani hapo jana kwa lengo la kumuunga mkono na kutaka akubali wamwakilishe kwenye kesi ya mauaji ya waandamanaji waliokuwa wanapinga utawala wake.

Kwenye taarifa yake, Mohamed Morsi ameendelea kusisitiza kuwa hautambui utawala wa kijeshi uliopo madarakani kwasasa na kwamba yeye bado ni kiongozi halali wa taifa hilo na ataendelea kushikilia msimamo wake.

Kiongozi huyo ameendelea kukashifu mapinduzi yaliyofanywa dhidi yake na kuwataka wananchi wanaomuunga mkono kutokubaliana na lolote ambalo wataelekezwa na utawala wa mpito kwakuwa rais halali yuko kizuizini kinyume cha sheria.

Morsi pia amekataa kuwakilishwa na wakili yeyote kwasasa akisisitiza kuwa haoni kama kuna haja ya kuwa na wakili kwasababu yeye anatambua kuwa bado ni rais halali aliyechaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Misri.

Kwenye mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari, mawakili waliomtembelea Morsi na washukiwa wengine, wamesema wao hawakwenda kama wanasiasa bali kama wanasheria ambao wanaona kuna haja ya kiongozi huyo kupata uwakilishi wakati huu akisubiri kesi yake kuanza kusikilizwa.

Hivi karibuni alipopandishwa kizimbani, Mohamed Morsi alikataa kujibu lolote hata wakati alipohojiwa na mwendesha mashtaka akisisitiza kuwa kinachofanywa sasa na mahakama ni kinyume cha sheria kwakuwa hawana mamlaka ya kumuhoji kiongozi aliyemadarakani kihalali.

Wachambuzi wa mambo wanahoji kuhusu utata wa kauli ya Morsi kuwa hataki kuwakilishwa na wakili yeyote kwasasa kwakuwa hatambui mapinduzi ya kijeshi, lakini itakuwaje atakapokubali kuwakilishwa na wakili wake? Je inamaanisha kuwa atatambua mapinduzi ya kijeshi? haya ni maswali ambayo wachambuzi wa mambo wanahoji kuhusu kauli ya Morsi.

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya ukiongozwa na mkuu wa sera za nje wa umoja huo walimtembelea rais Morsi miezi kadhaa iliyopita na kueleza kuridhishwa na namna alivyokuwa akihifadhiwa licha ya kutoa wito wa kupatikana kwa suluhu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.