Pata taarifa kuu
KENYA-RAILA ODINGA-UHURU KENYATTA

Odinga asisitiza hatambui uongozi wa rais Kenyatta, aikashifu Marekani

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA, Raila Odinga, amesisitiza kuwa hatambui rais Uhuru Kenyatta kama kiongozi halali wa taifa hilo.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga REUTERS/Baz Ratner
Matangazo ya kibiashara

Odinga amesema yeye na muungano wake, hautambui Uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Kiongozi huyo wa NASA, aliojiondoa kwa kile alichokisema uwanja haukuwa sawa kwa zoezi hilo kuwa huru na haki na kukubalika.

Kauli hii ya Odinga inakuja wakati huu, muungano wake ukitarajiwa “kumwapisha” wiki ijayo, kama rais wa watu.

Mpango huo umeendelea kuzua wasiwasi nchini humo na hata Marekani kupitia Balozi wake Robert Godec, akimtaka Odinga kuachana na mpango wa kumwapisha.

Wachambuzi wa siasa nchini Kenya wanasema hakuna shaka kuwa kisheria, Uhuru Kenyatta aliapishwa kisheria lakini suala tata linalosalia ni uhalali wa Kenyatta ambaye anaonekana kutokubalika katika ngome nyingi za upinzani.

“Kuapishwa kwa Kenyatta kulifanyika kwa kisheria na kwa mujibu wa Katiba, ila changamoto kubwa ipo katika kukubalika kwake, na hivyo hili ni tatizo la kisiasa,” Wakili Daktari Alutalala Mukhwana.

Katika hatua nyingine, Odinga ameiambia Marekani kuacha kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo na kuwaacha Wakenya wenyewe kutatua changamoto zinazowakabili.

“Changamoto za Kenya zitatatuliwa na Wakenya wenyewe,” alisema.

Odinga ameiambia Marekani kuwa inaweza kutoa ushauri kwa Wakenya lakini haiwezi kuwaamulia cha kufanya.

"Ikiwa mnataka kutushauri sawa, ila lifanye kwa siri," aliongeza.

Msemaji wa Odinga Salim Lone amesema kiongozi huyo yuko tayari kwa mazungumzo na rais Kenyatta lakini ajenda kuu iwe ni kupatikana kwa haki ya Uchaguzi.

Mbali na suala hilo, Odinga ameushtumu uongozi wa rais Kenyatta kwa kutumia polisi kuwauwa wafuasi wake 215 wakiwemo watoto, kipindi chote cha Uchaguzi mwaka huu.

Polisi wamekanusha kuhusika na mauaji hayo.

Odinga siku ya Alhamisi, aliongoza hafla ya kuaga miili ya wafuasi wake waliopoteza maisha katika makabiliano na polisi hivi karibuni.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.