Pata taarifa kuu
UTURUKI-TANZANIA

Erdogan aiomba Tanzania kuzuia harakati za chama cha Fethullah

Rais wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan, amemuomba mwenzake wa Tanzania, John Pombe Magufuli, kumsaidia katika mapambano ya ugaidi na hasa kuenea kwa vuguvugu la chama cha Fethu, linaloongozwa na mwanasiasa mkongwe wa nchi hiyo, Fethullah Gülen.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, akizungumza ikulu Dar es Salaam, alipokutana na rais wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan. Januari 23, 2017
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, akizungumza ikulu Dar es Salaam, alipokutana na rais wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan. Januari 23, 2017 Screenshot/AzamTV
Matangazo ya kibiashara

Kwenye hotuba yake, rais Erdogan amemueleza rais Magufuli kile ambacho kilishuhudiwa nchini mwake mwezi Julai mwaka jana, ambapo maofisa kadhaa wa jeshi walijaribu kuipindua Serikali yake.

Rais Erdogan amesema kuwa, Serikali yake inao ushahidi wa kutosha kuhusu watu waliohusika kwenye jaribio lile, na kwamba ana imani Serikali ya Tanzania itaisaidia nchi yake katika kukidhibiti chama cha Fethu, alichosema kinaeneza propaganda mbaya dhidi ya Uturuki.

Vuguvugu la Fethullah Gülen, linaendesha na kufadhili shule za fedha nchini Tanzania, na wadadisi wa mambo wanaona kuwa ziara yake imelenga kujaribu kuishawishi nchi ya Tanzania kusitisha ushirikiano na kiongozi huyo wanayedai alishiriki njama za kuipindua Serikali yake.

Rais wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan, alipokuwa Tanzania
Rais wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan, alipokuwa Tanzania Screenshot/AzamTV

Kwa upande wake rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, ameipongeza nchi ya Uturuki kwa kuendeleza ushirikiano wao, ambapo amesema wamekubaliana na mwenzake kuongeza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili.

Ufadhili wa Serikali ya Uturuki kwa Serikali ya Tanzania, unakadiriwa kufikia kiasi cha dola za Marekani milioni 150, na rais Erdogan amesema kiasi hiko kitaongezeka hadi kufikia dola milioni 500.

Katika ziara hiyo, nchi hizi mbili zimetiliana saini mikataba 9 ya ushirikiano, ikiwemo ile ya kiuchumi, miundombinu, elimu, biashara, afya na mawasiliano hasa ushirikiano wa kati ya televisheni ya taifa ya Uturuki na ile ya Tanzania, TBC.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.