Kigali yakashifu matamshi ya Bujumbura dhidi yake
Nairobi – Serikali ya Rwanda kupitia taarifa kwenye mtandao wa X, imekashifu matamshi yaliotolewa na rais wa Burundi Evariste Ndayishimye wikendi iliopita akiwa jijini kinshasa nchini DRC, ambayo inasema yalilenga kuchochea mgawanyiko miongoni mwa vijana raia wa Rwanda na kuhatarisha amani na usalama katika ukanda wa maziwa makuu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Kwa mujibu wa taarifa ya Kigali, raia wa Rwanda wanafanya bidi kuimarisha umoja na maendeleo na kwamba kwa mtu yeyote kujaribu kuwataka vijana wa taifa hilo kupindua serikali yao ni jambo la kukera.
AMAKURU AGEZWEHO
— Rwanda Broadcasting Agency (RBA) (@rbarwanda) January 22, 2024
Guverinoma y'u Rwanda yatangaje ko ibabajwe n'amagambo agumura yavuzwe na Perezida w’u Burundi, Evariste Ndayishimiye, i Kinshasa tariki 21 Mutarama 2024.
Muri iri tangazo, u Rwanda ruvuga ko kuba umukuru w'igihugu cy'igituranyi yavuga amagambo ahamagarira… pic.twitter.com/znQ8fF5ZgH
Aidha Kigali imeeleza kuwa ilikuwa makosa kwa kwa kiongozi wa nchi jirani kutoa matamshi kama hayo katika hafla ya umoja wa Afrika suala ambalo ni ukiukaji wa mkataba wa Umoja huo.
Vilevile utawala wa Kigali umeeleza kuwa hauna haja ya kuzua ghasia na majirani zake na kwamba Rwanda itaendelea kushirikiana na mataifa jirani katika eneo hili na kwengineko kuimarisha udhibiti na maendeleo.
Katika mahojiano na vijana siku ya Jumapili mjini Kinshasa, rais Ndayishimiye alikosoa mamlaka ya Rwanda kwa kusaidia kile ambacho alitaja kuwa makundi yanayovuruga eneo hilo.
Aidha rais Ndayishimiye alisema kuwa ilikuwa muhimu kuendeleza mapambano hadi raia wa Rwanda wenyewe waanze kutoa shinikizo ambapo aliongeza kuwa anadhani hata vijana wa Rwanda hawawezi kukubali kuwa wafungwa katika eneo hilo.
Tangu mwaka uliopita, uhusiano kati ya Bujumbura na Kigali umekuwa ukiyumba baada Burundi kuituhumu Rwanda kwa kusaidia kundi la RED-Tabara lililofanya shambulio baya kaskazini na magharibi mwa nchi yake.
Kwa upande wake, serikali ya Rwanda imeendelea kusema haina uhusiano wowote na shambulio hilo.
Tayari Burundi imetangaza kufunga mpaka wake na jirani yake Rwanda hatua inayokuja wakati huu mzozo kati ya mataifa hayo ukionekana kuongezeka.