Pata taarifa kuu

Rwanda :Maombolezo yanaendelea kufuatia vifo vya raia zaidi ya 130 katika mafuriko

NAIROBI – Raia wa Rwanda wameendelea na maombolezo kufuatia vifo vya watu zaidi ya 130, waliofariki kutokana na mafuriko yaliyokumba eneo la magharibi mwa nchi hiyo, ambapo mamia ya nyumba zimeharibiwa.

Raia katika eneo la  Rubavu nchini Rwanda waliopoteza makazi yao katika mafuriko ,Tarehe 3 Mei 2023.
Raia katika eneo la Rubavu nchini Rwanda waliopoteza makazi yao katika mafuriko ,Tarehe 3 Mei 2023. © Jean Bizimana / Reuters
Matangazo ya kibiashara

Maombolezo haya yanafanyika wakati huu Serikali ikiendelea kukadiria hasara iliyotokana na mafuriko hayo, huku shughuli za mazishi pia zikiendelea katika moja ya majanga mabaya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo.

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Rwanda, zilisababisha kutokea kwa maporomoko ya udongo yaliyoharibu nyumba na miundombinu mingine kama barabara, hasa katika eneo la magharibi mwa nchi linalopakana na ziwa Kivu ambako kumeripotiwa maafa zaidi.

Maporomoko ya udongo yameharibu miundo mbinu nchini Rwanda
Maporomoko ya udongo yameharibu miundo mbinu nchini Rwanda AFP - MARIAM KONE

Baadhi ya familia zimeeleza namna zilivyopoteza ndugu zao, baadhi kama Anonciata, anasema amepoteza mtoto wake baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo na kuta za nyumba yake na alifariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini katika wilaya ya Karongi.

Aidha wengine mbali na kupoteza ndugu zao, wamesema shughuli za maisha ya kawaida zimekoma rasmi baada ya kupoteza mali nyingi ambazo walikuwa wakizitegemea kukimu familia zao.

Tangu Mei 2 maeneo ya kaskazini, magharibi na kusini mwa Rwanda, yameshuhudia mafuriko yaliyosababisha maafa kwa raia, huku miongoni mwa waliofariki wakiwemo wanafunzi 15 na shule 33 kuharibiwa.

Inahofiwa kuwa huenda idadi ya waathiriwa wa mafuriko na maporomoko ya udongo ikaongezeka wakati huu mvua kubwa ikiendelea kunyesha katika maeneo ya Magahribi ya Kaskazini ya Rwanda
Inahofiwa kuwa huenda idadi ya waathiriwa wa mafuriko na maporomoko ya udongo ikaongezeka wakati huu mvua kubwa ikiendelea kunyesha katika maeneo ya Magahribi ya Kaskazini ya Rwanda REUTERS - JEAN BIZIMANA

Vifo vya wanafunzi viliripotiwa kwenye miji ya Karongi, Nyabihu, Ngororero na Rubavu, ambapo tayari baadhi wamezikwa huku shirika la msalaba mwekundu nchini humo likiendelea kuwasaidia waathirika.

Eugene Kanangwa, ni mkuu wa kitengo cha dharura cha shirika la msalaba mwekundu nchini Rwanda.

“Tunaendelea kuwasaidia watu walioathirika na mafuriko hapa katika eneo la Rubavu, waathiriwa wanasaidiwa kwa kupewa bidhaa mbali mbali za kuwasaidia wakati huu.” Alisema Eugene Kanangwa, mkuu wa kitengo cha dharura cha shirika la msalaba mwekundu nchini Rwanda

00:44

Eugene Kanangwa, kuhusu hali ya mafuriko nchini Rwanda

Tayari Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, wameanza kutoa misaada kwa raia walioathirika, ikiwemo makazi ya muda, chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.