Pata taarifa kuu
DRC

DRC: Waasi wa M23 waruhusu usafiri wa magari kutoka kwenye miji wanayodhibiti

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,  waasi wa M 23 wameruhusu safari za magari kutoka miji wanayodhibiti ya Rutshuru na Kiwanja, kwenda katika maeneo mengine ya jimbo la Kivu Kaskazini  kama Goma.

DRC: Dereva wa lori la mizigo baada ya kuwasili mjini Goma akitokea Kiwanja baada ya kuruhusiwa na waasi wa M 23 (07/12/2022)
DRC: Dereva wa lori la mizigo baada ya kuwasili mjini Goma akitokea Kiwanja baada ya kuruhusiwa na waasi wa M 23 (07/12/2022) © FMM- Tschube Ngorombi
Matangazo ya kibiashara

Hii imekuja baada ya waasi hao kusema wako tayari kuondoka katika maeneo hayo, iwapo watashiriki kwenye mazungumzo ya amani na serikali ya DRC.

Msemaji wa waasi hao Willy Ngoma, ameiambia RFI Kiswahili kuwa, safari hizo zimeanza siku ya Jumatano baada ya kuzuiwa kwa karibu mwezi mmoja.

“Ni kweli, tumeruhusu safari hizo kuanza, hakuna mtu atakayewasumbua,” amesema.

Dereva wa lori la mizigo, aliyekuwa wa kwanza kufika Goma kutoka Kiwanja, katika mazungumzo na mwandishi wetu Chube Ngorombi, amesema njiani alikutana na kusimamishwa na waasi hao, lakini akaruhusiwa kupita.

“Nilianza safari kutoka Kiwanja asubuhi, nilikutana na waasi wa M 23 huko Rugari, wakaniruhusu kupita,” amesema dereva huyo.

00:45

Dereva wa Lori aliyetoka Kiwanja kwenda Goma

Aidha, ameeleza kuwa malori mengine ya mizigo kutoka nchi jirani kama Uganda, yameruhusiwa kuondoka Kiwanja.

Katika hatua nyingine, waasi wa M 23 wamesema wako tayari kwa ajili ya mazungumzo na kuomba kukutana na mratibu wa mazungumzo kutoka jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki, rais wa zamani wa  Kenya Uhuru Kenyatta.

“Tuko tayari kuondoka, lakini tutaenda wapi, tunataka mazungumzo, tunapenda amani, “ amesema Willy Ngoma.

02:35

Mahojiano kati ya Victor Abuso na msemaji wa M 23 Willy Ngoma

Wito wa M 23 unakuja kuelekea mazungumzo mengine ya amani mwezi Januari mjini Goma, baada ya kumalizika kwa yale ya Nairobi wiki hii, na waasi kukubali kuweka silaha chini. Waasi wa M 23 hawakualikwa katika mazungumzo hayo.

Serikali ya Kinshasa, inawashtumu waasi hao kwa kuwauwa raia karibu  300 katika kijiji cha Kishishe mwishoni mwa mwezi Novemba, madai ambayo waasi hao wanakanusha.

Uongozi wa rais Felix Tshisekedi, unasema waasi wa M 23 ni magaidi, na kuishtumu nchi jirani ya Rwanda kuwaunga mkono.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.