Pata taarifa kuu
KENYA-KATIBA-MAHAKAMA

Mahakama ya rufaa nchini Kenya yatupilia mbali mchakato wa kurekebisha Katiba BBI

Mahakama ya rufaa nchini Kenya, imeunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu, kuwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini humo maarufu kama BBI, ni kinyume cha Katiba ya nchi hiyo na kutupilia mbali, rufaa iliyowasilishwa kutaka maamuzi hayo kubadilishwa.

Majaji wa Mahakama ya Juu nchini Kenya , 28/08/2017
Majaji wa Mahakama ya Juu nchini Kenya , 28/08/2017 REUTERS/Baz Ratner
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo umetolewa na Majaji Sita kati ya Saba waliokuwa wanasikiliza kesi ya rufaa iliyokuwa imewasilishwa na wanaounga mkono mchakato huo.

Wakiongozwa na Jaji Daniel Musinga rais  wa Mahakama hiyo, wamemshtumu rais Uhuru Kenyatta kwa kwenda kinyume cha Katiba kwa kuanzisha mchakato huo.

Mchakato wa kutaka kuibadilisha Katiba ya nchi hiyo iliyopatikana mwaka 2010, ulianza baada ya rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kumaliza uhasama wao kisiasa na kuungana ili kubadilisha mfumo wa uongozi nchini humo.

Kenyatta na Odinga wamekuwa wakisema  mabadiliko ya katiba yalikuwa muhimu ili kuliunganisha taifa hilo hasa wakati wa kisiasa, serikali kuwa shirikishi kwa kuunda wadhifa wa Waziri Mkuu na Manaibu wawili wa rais.

Baada ya maamuzi hayo, Odinga ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema anakubaliana na uamuzi wa Mahakama na mchakato wa kuibadilisha Katiba hiyo utaendelea wakati mwingine.

Huu unaonekana ushindi kwa wanasiasa waliokuwa wanapinga mchakato huo, wakiongozwa na naibu Rais William Ruto ambaye ameweka nia ya kuwania urais mwaka 2022.

Iwapo hakutakuwa na rufaa nyingine kwenda  kwenye Mahakama ya Juu, ratiba ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Agosti 9 mwaka 2022 itasalia kama ilivyo kwa sababu hakutakuwa na kura ya maamuzi.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa, baada ya uamuzi huu, sasa mirengo ya kisiasa itaanza kujitokeza kwa lengo la kutaka kuunda serikali mwaka 2022.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.