Pata taarifa kuu
Burundi-UN-Siasa

Umoja wa Mataifa umeionya Serikali ya Burundi kutotumia ubabe kwa kukandamiza upinzani na vyama vya kiraia

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon ameionya serikali ya Burundi kuhusu kuendelea kuminywa kwa uhuru wa kujieleza na haki ya kufanya mikusanyiko ambapo ametoa wito kwa serikali na vyama vya siasa kujiepusha na harakati zozote ambazo zinaweza kuchangia kutokea machafuko.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon RFI
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msemaji wa katibu mkuu Ban, imesema kuwa kiongozi huyo ameguswa na hali tete ya kisiasa inayoendelea kushuhudiwa nchini humo kati ya wanaharakati wa upinzani na polisi.

Katibu mkuu Ban amelaani hatua ya Serikali kukataza mikusanyiko ya kisiasa ya vyama vya upinzani na hatua ya polisi kutumia nguvu dhidi ya wapinzani huku kundi la vijana wa chama tawala wakipewa nafasi ya kufanya mikusanyiko.

Kiongozi huyo amesema ili nchi ya Burundi ifanye uchaguzi ulio huru na haki ifikapo mwaka 2015 ni lazima serikali uruhusu uhuru wa demokrasia kwa kutoa fursa sawa kwa upinzani.

Onyo hilo la katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa linakuja, baada ya kutokea kwa makabilioano mwishoni mwa juma liliyopita kati ya polisi na wafuasi wa chama cha upinzani cha MSD, huku vyombo vya sheria nchini humo vikitoa hati ya kumkamata kiongozi wa chama hicho Alexis Sinduhije, vikimtuhumu kukaidi amri ya viongozi na kujihusisha na kundi lenye silaha liliyoanzishwa dhidi ya utawala.

Wafuasi 71 wa chama cha MSD walikamatwa jumamosi iliyopita.

Wafuasi ho wa chama cha MSD akiwemo kiongozi wa chama hicho, Alexis Sinduhije wanakabiliwa na adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Makabiliano kati ya wafuasi wa chama cha MSD na polisi yaliyodumu zaidi ya saa moja, yalisababisha wafuasi 20 wa chama hicho kujeruhiwa kwa risase, wakiwemo askari polisi watanu.

Chanzo cha makabiliano hayo ni polisi kuwatawanya wafuasi wa chama cha MSD, ambao walikua katika mazoezi ya kunyoosha misuli hapo jumamosi, zaidi ya wafuasi 200 walikimbilia katika makao makuu ya chama hicho na kuwateka askari polisi wawili.

Kwa zaidi ya miaka 4 sasa, utawala nchini Burundi umekua ukipiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vinavyojumuika katika muungano wa vyama vya upinzani ADC-IKIBIRI, pamoja na maandamano ya vyama hivyo na mashirika ya kiraia.

Vyama hivyo vya upinzani vimekua vimekua vikitishia kuanzisha maadamano, vikibaini kwamba vinafanyiwa unyonge.

Hayo yakijiri, chama cha UPRONA, ambacho kina wafuasi wengi kutoka jamii ya watutsi na ni chama kimoja pekee kiliyoshiriki chaguzi za mwaka 2010 pamoja na chama cha CNDD-FDD, kilijiondoa serikalini hivi karibuni , baada ya viongozi wa chama hicho kubaini kwamba utawala wa CNDD-FDD umekua ukijaribu kukisambaratisha kutokana na msimamo wake wa kupinga marekebisho ya katiba.

Hivi karibuni mkuu wa sera za nje wa umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, amesema kwamba anatiwa wasiwasi na hali ya kisiasa inayoendelea nchini Burundi, huku akizitaka pande zote husika kuketi kwenye meza ya mazungumzo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Burundi (BNUB), imebaini kwamba matukio yaliyotokea jumamosi yanaonesha kuwa hali ya kisiasa inaendelea kuwa mbaya wakati kukisalia miezi kadhaa ili chaguzi za mwaka 2015 zifanyike.

Marekani, kwa upande wake, imeendelea kulani vikali mwenendo wa polisi wa kutumia nguvu dhidi ya upinzani, pamoja na kitendo cha wafuasi wa MSD cha kuwateka kuwateka askari polisi.

Burundi ni taifa ambalo limetoka mwaka 2006 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe viliyodumu zaidi ya miaka 10, na kusababisha watu 300,000 kupoteza maisha na mamia kwa maelfu kuyahama makaazi yao.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.