Pata taarifa kuu
UFARANSA-JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

Ufaransa kuongeza wanajeshi 400 zaidi nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati

Ufaransa ina mpango wa kuongeza wanajeshi mia nne zaidi ili kuimarisha oparesheni za kiusalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Rais wa nchi hiyo, Francois Hollande amesema Paris inaongeza idadi hiyo ili kufikisha wanajeshi 2000 nchini humo.

Waasi wa Seleka ni miongoni mwa makundi ya wapiganaji wanaozorotesha usalama mjini Bangui
Waasi wa Seleka ni miongoni mwa makundi ya wapiganaji wanaozorotesha usalama mjini Bangui REUTERS/Siegfried Modola
Matangazo ya kibiashara

Rais Hollande pia ameutaka Umoja wa Ulaya EU kuharakisha mpango wa upelekaji wa wanajeshi wake 500 huku akiahidi kuwa serikali yake itaendeleza jitihada za kukomesha mauaji, unyanyasaji na kurejesha usalama.

Kwa upande wake Mkuu wa sera za nje wa EU, Catherine Ashton amesema wamejipanga kutekeleza ahadi hiyo na kuwa wanajeshi hao watawasili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati hivi karibuni.

Wanadiplomasia wa Ulaya wanasema majeshi hayo yataanza kuingia mjini Bangui mwezi ujao, baada ya mapema juma hili Mawaziri wa EU kuipa oparesheni hiyo muda wa miezi tisa.

Mbali na Ufaransa, nchi tano wanachama wa EU wamejitolea kushiriki mpango huo, wakati mataifa makubwa kama Uingereza na Ujerumani yakikataa kuahidi iwapo yataoa wanajeshi wake kwenye oparesheni hiyo.

Jitihada hizo zinakuja wakati shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF likisema watoto 133 wameuawa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, baadhi yao wamechinjwa na wengine wamebaki na ulemavu.

Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa katika machafuko toka Muungano wa waasi wa Seleka ulipomuondoa madarakani Rais Francois Bozize mwezi Machi mwaka jana na kumuweka madarakani kiongozi wao wa kiislamu Michel Djotodia aliyejiuzulu kwa shinikizo mwezi uliopita.

Rais mpya wa mpito Catherine Samba Panza ameahidi kukabiliana na makundi ya wapiganaji likiwemo la Kikristo la anti-balaka ambalo limekuwa likituhumiwa kwa uvunjifu wa amani.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.