Pata taarifa kuu
SUDAN

Serikali ya Sudan yapinga taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii juu ya mauaji ya waandamanaji

Serikali ya Sudan imekanusha madai ya wao kuhusika kwenye mauaji ya wananchi wake wanaoendelea kufanya maandamano ya kupinga mpango wa kuongezwa kwa tozo ya ruzuku iliyosababisha kuongezwa kwa bei ya mafuta kitu kilichowachukiza wananchi wakisema hali hiyo inachangia uwepo wa hali ngumu ya maisha.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Sudan Ibrahim Mahmoud Hamed akizungumza na wanahabari juu ya maandamano yanayoendelea nchini mwake
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Sudan Ibrahim Mahmoud Hamed akizungumza na wanahabari juu ya maandamano yanayoendelea nchini mwake
Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Khartoum imeweka bayana picha ambazo zimekuwa zikioneshwa na Mashirika ya Kutetea Binadamu na Vyama Vya Upinzani si za kweli na zimekuwa zikitengenezwa kwa lengo la kuonesha Utawala wa Rais Omar Hassan Ahmed Al Bashir ni wa kikatili dhidi ya wananchi wake.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Sudan Ibrahim Mohamoud Hamed amesema picha nyingi ambazo zimekuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamaii hasa youtube na facebook si za kweli na zimekuwa zikiendelea kutolewa kwa lengo maalum la kutaka kuonesha Serikali iliyopo madarakani ni katili.

Hamed amewaambia wanahabari picha hizo zimekuwa zikisambazwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii nchini Misri na wala hazijapigwa nchinio Sudan kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na wasambazaji aliowatuhumu wamekuwa na lengo baya na nchi hiyo.

Waziri Hamed amesema licha ya maandamano hayo kudumu kwa siku nane na kuchangia hasara kubwa ikiwemo kuchomwa kwa vituo vya kuuzia mafuta, kuharibiwa kwa maduka na kuchomwa moto kwa magari lakini Jeshi limekuwa likitumia nguvu za kadri.

Serikali imesema Jeshi la Sudan limekuwa makini sana kwenye mkakati wake wa kuzima maandamano hayo yaliyochukuliwa na Wapinzani kama sehemu yao ya kutaka kuuangusha Utwala uliopo madarakani.

Marekani yenyewe imetoa wito kwa pande zinazohasimiana nchini Sudan kuhakikisha zinasaka suluhu na hatimaye kumaliza hali hiyo ya machafuko inayochangia wananchi kupoteza maisha kila uchao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry ametoa kauli hiyo alipokutana na mwenzake wa Sudana Ali Karti licha ya kwamba hawakuingia kwa undani kuzungumzia suala hilo la maandamano hayo baya zaidi kutokea nchini humo.

Katika hatua nyingine Waziri wa Uingereza anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mark Simmonds amekiri kushtushwa na taarifa za kuwa Jeshi nchini Sudan limekuwa mstari wa mbele kuwapiga risasi na kuwaua waandamanaji.

Vyombo vya Habari hasa Gazeti la Al Youm Al Taly limeendelea kuishutumu serikali kufanya mauzji ya wananchi wanaoendelea kuandamana licha ya yenyewe kuendelea kukanusha vikali.

Hadi sasa kumekuwa na takwimu tofauti za watu waliopoteza maisha kwani serikali inasema watu thelathini na wanne wamepoteza maisha lakini Upinzani na Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu yanadai zaidi ya watu hamsini wameuawa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.