Pata taarifa kuu
JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-AFRIKA KUSINI-DRC-UN

Waasi wa Seleka waahidi kutekeleza mkataba waliotiliana saini na Serikali licha ya kuingia Bangui

Waasi wa Seleka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wamefanikiwa kuutwaa mji mkuu Bangui huku rais wa nchi hiyo Francois Bozize akikimbilia nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC. 

Wanajeshi wa Seleka wakipita katika mitaa ya mji wa Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wanajeshi wa Seleka wakipita katika mitaa ya mji wa Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati Reuters
Matangazo ya kibiashara

Makundi ya wanajeshi waasi yalionekana kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Bangui saa chache kabla ya kuvamia ikulu ya nchi hiyo na kutangaza kuipindua Serikali ya rais Bozize.

Kiongozi wa kundi la Seleka, Michel Djotodia ameiambia idhaa ya redio Ufaransa RFI kuwa kundi lake litaheshimu makubaliano ambayo walitiliana saini na Serikali na kwamba wataheshimu mkataba huo.

Djotodia ameongeza kuwa wamefanya mazungumzo na waziri mkuu mteule, Nicolas Tiangaye na kukubaliana aendelee kuongoza Serikali wakati huu ambapo akuna rais.

Wakati waas hao wakiingia mjini Bangui, wanajeshi kadhaa wa Afrika Kusini wameripotiwa kupoteza maisha wakati wa makabiliano na waasi wa Seleka waliokuwa wakiingia mjini humo.

Brigedia Jenerali, Xolani Mabanga wa vikosi vya Afrika Kusini vilivyoko nchini Jamhuri ya Afrika ya kati amethibitisha wanajeshi kadhaa kujeruhiwa ingawa hakutoa idadi yoyote iwapo kuna wanajeshi waliopoteza maisha.

Kabla ya kuingia mjini Bangui, waasi hao walitoa siku tatu kwa rais Bozize kuondoka madarakani ambapo mara baada ya kiongozi huyo kukaidi ndipo walipoamua kuingia kwa nguvu.

Rais Bozize kwa sasa anapatiwa hifadhi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC.

Jumuiya ya Kimataifa imelaani tukio lililofanywa na waasi wa Seleka, ambapo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon ametaka waasi hao kuheshimu katiba ya nchi hiyo.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.