Pata taarifa kuu
MALI-UFARANSA

Jeshi la Mali latuhumiwa kutekeleza unyanyasaji na mauaji dhidi ya raia wanaowatuhumu kushirikiana na Makundi ya Kiislam

Jeshi la Mali limeingia lawamani likitajwa kutekeleza unyanyasaji, mauaji na mateso kwa wakazi wa Kaskazini mwa Taifa hilo kwa madai ya kuendelea kuwasaka Wapiganaji wa Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanashikia hatamu ya eneo hilo.

Wanajeshi wa Mali wakiwa na Watu waliokamatwa katika Mji wa Gao wakihusishwa kuwa na uhusiano na Kundi la MUJAO
Wanajeshi wa Mali wakiwa na Watu waliokamatwa katika Mji wa Gao wakihusishwa kuwa na uhusiano na Kundi la MUJAO REUTERS/Joe Penney
Matangazo ya kibiashara

Wakazi wa Kaskazini mwa Mali wameelekeza lawama zao kwa Jeshi la Mali wakisema limekuwa likinyanyasa na kufanya mauaji dhidi ya watu wasio na hatia kwa kisingizio wamekuwa wakiyasaidia Makundi ya Kiislam.

Madai hayo yamethibitishwa na Madaktari, Waandishi wa Habari, Jeshi la Mali na lile la Ufaransa ambalo limesema kumekuwa na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya raia ambao wamekuwa wakihusishwa na Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanatawala eneo hilo.

Jeshi la Mali limekuwa likitajwa kufanya mauaji ya wananchi wa eneo la Kaskazini wakiwatuhumu kuwa na uhusiano na Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yamekita kambi kwa kipindi cha miezi tisa.

Mkuu wa Kikosi cha Polisi huko Gao Kanali Saliou Maiga amethibitisha kupokea malalamiko hayo ya kufanyika vitendo vya mateso na mauaji vinavyofanywa na wanajeshi wao huko Kaskazini.

Kanali Maiga ameongeza kuwa wamebaini kesi nyingi ambazo zinawahusisha wanajeshi wao kufanya vitendo ambavyo vinakiuka haki za binadamu na wanaendelea kuzifanyia kazi taarifa hizo.

Tuhuma za uwepo wa mateso na mauaji dhidi ya raia ziliongezeka tangu Jeshi la Ufaransa lilivyofanya uvamizi wa kijeshi ambapo kwenye shambulizi lao moja walikiri kuwaua wananchi watatu na kuiwajeruhi wengine kumi na watano.

Makundi ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Mali yamekuwa yakilalama juu ya vitendo vya utesaji na mauaji vinavyofanywa na wanajeshi wa taifa hilo Kaskazini mwa Taifa hilo na kuitaka serikali kuchukua hatua.

Katika hatua nyingine Umoja wa Ulaya EU unatarajiwa kutoa mafunzo kwa wanajeshi 2,500 wa Mali kuanzia mwezi Aprili lengo likiwa ni kuwaweka tayari kwa ajili ya kuchukua jukumu la ulinzi pindi majeshi ya Ufaransa yatakapoondoka.

Mkuu wa Operesheni ya Umoja wa Ulaya ya Mafunzo EUTM Jenerali Francois Lecointre amesema lazima wawaandae wanajeshi wa Mali kwa kazi ya kulinda amani na kuweza kukabiliana na Makundi hatari yanayopatikana Kaskazini mwa Taifa hilo.

Jenerali Lecointre amesema mafunzo hayo yatakuwa ya miezi miwili ambapo yatahusishwa wanajeshi 650 hadi 700 kila wakati ahtua ambayo imeafikiwa na Mkuu wa Majeshi ya Mali Jenerali Ibrahima Dahirou Dembele.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.