Pata taarifa kuu
SYRIA-URUSI

Hali inazidi kuwa mbaya nchini Syria na kushuhudia watu 10 wakiuawa kwenye shambulizi la kigaidi Damascus

Mgogoro ambao unaendelea nchini Syria umetajwa kuwa mbaya na unaendelea kuleta madhara zaidi kipindi hiki ambacho Televisheni ya taifa nchini humo ikithibitisha watu kumi wamepoteza maisha baada ya kutekeleza kwa shambulizi la kigaidi kwenye Jiji la Damascus. Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi amesema hali inazidi kuwa mbaya lakini hawatokatishwa tamaa na kile akinachoshuhudiwa na badala yake watapambana kuhakikisha wanarejesha utulivu katika Taifa hilo linaloshuhudiwa mapigano kwa miezi ishirini sasa.

Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov baada ya mkutano wao
Mpatanishi wa Mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergie Lavrov baada ya mkutano wao
Matangazo ya kibiashara

Brahimi akiwa nchini Urusi ambako amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Moscow Sergei Lavrov amesema kila kukicha hali ya usalama inazidi kuzorota nchini Syria kutokana na mashambulizi ambayo yanafanywa na pande mbili zinazohasimiana kwa kipindi hiki chote.

Mpatanishi huyo ameelekea nchini Urusi kusaka uungwaji mkono kutoka kwa taifa hilo ambalo linauhusiano mzuri na Utawala wa Syria chini ya ris Bashar Al Assad huku likiendelea kuhimiza suluhu ya mgogoro itapatikana kwa wapinzani kuweka silaha zao chini.

Brahimi amesema mapigano yamezuka upya baada ya kusitishwa wakati wa sherehe za Sikukuu ya Eid Al Adha lakini kwa sasa mashambulizi yamekuwa makali zaidi na kile kinachoweza kutokea ni kuibuka kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi hiyo.

Lavrov kwa upande wake amemwambia Brahimi nchi yake imekatishwa tamaa kutokana na wapinzani kuvunja makubaliano yaliyokuwa yamewekwa kutokana na wao kuanzisha mapigano upya na kuwa chanzo cha kuibuka kwa mauaji zaidi ya watu wasio na hatia.

Katika hatua nyingine Televisheni ya taifa imeonesha picha zinazoonesha shambulizi hilo la kigaidi lililosababisha vifo vya watu watatu baada ya mtu mwenye bomu kujilipua katikati ya watu waliokuwa kwenye Jiji la Damascus.

Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban Ki Moon ameonesha kuchanganyikiwa kutokana na kushindwa kumalizwa kwa mapigano kama ambavyo pande zote zilivyoahidi kufanya hivyo.

Ban amekiri kutokuelewa ni kwa nini pande ambazo zinahasimiana zimeshindwa kuweka silaha chini kama ambavyo alipendekeza Mpatanishi wa Mgogoro huo Brahimi anayeendelea kusaka uungwaji mkono wa kumaliza umwagaji wa damu.

Takwimu za Makundi ya Kutetea Haki za Binadamu zinaonesha watu zaidi ya elfu thelathini na tano wamepoteza maisha tangu nchi hiyo iingie kwenye machafuko ambayo yamezidi kusonga mbele.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.