Pata taarifa kuu
SYRIA

Mashirika ya Misaada yaanza kutoa huduma kwa Wakazi wa Homs wakati huu Ufaransa ikifunga Ubalozi wake huko Damascus

Mashirika ya Misaada kutoka Mwezi Mwekundu na Shirika la Msalaba Mwekundu yameingia katika Jiji la Homs nchini Syria katika Wilaya ya Nana Amr na kuanza kutoa huduma kwa waathirika wa mashambulizi ambayo yamekuwa yakifanyika kati ya wapinzani na wanajeshi watiifu wa Rais Bashar Al Assad. Huduma hizo zimeanza kuwafikia mamia ya wananchi walioathirika na mapigano makali ambayo yamedumu kwa majuma kadhaa sasa bila ya kupatikana kwa suluhu yoyote huku idadi ya vifo ikiongezeka kila uchao.

Moshi ambao unatokana na mashambulizi ya mabomu yanayotekelezwa katika Jiji la Homs kuwalenga wapinzani wa serikali
Moshi ambao unatokana na mashambulizi ya mabomu yanayotekelezwa katika Jiji la Homs kuwalenga wapinzani wa serikali Reuters
Matangazo ya kibiashara

Taarifa zinasema kuwa watu thelathini na watano wamepoteza maisha wakiwemo kumi kutoka katika Jiji la Homs ikiwa ni muendelezo wa mapigano ambayo yameendelea kuzidi kuchacha katika nchi hiyo.

Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu nchini Syria Rami Abdel Rahman amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo licha ya huduma za misaada kuendelea kuwafikia maelfu ya wananchi walioathirika na mapigano hayo.

Haya yanakuja wakati huu ambapo Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy akitangaza kumrejesha nyumbani Balozi wa nchi hiyo na kufunga ofisi za Ubalozi wao huko Damascus kutokana na kuendelea kwa umwagaji wa damu.

Mapema Majeshi Tiifu kwa Rais wa Syria Bashar Al Assad yamerudishwa nyuma kwenye Wilaya ya Baba Amr iliyopo katika Jiji la Homs baada ya Waasi kujipanga upya na kufanikiwa kurejesha tena eneo hilo kwenye himaya yao.

Baraza la Taifa la Waasi Nchini Syria SNC limethibitisha wapiganaji wake kufanikiwa kuichukua tena Wilaya ya Baba Amr baada ya hiyo jana kuchukuliwa na Jeshi la Syria lakini pia wameonya kutakuwa na umwagaji mkubwa wa damu iwapo mapambano hayo yanateendelea.

Taarifa hizi zimetolewa wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN likitaka mapigano yasimame na hivyo kuruhusu misaada kuwafikia waathirika wanaohitaji huduma za haraka za kibinadamu hasa katika Jiji la Homs linaloshuhudia mashambulizi ya mabomu.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kwenye taarifa yake limethibitisha China na Urusi kuunga mkono azimio hilo la kusitishwa kwa mapigano ili misaada iweze kuwafikia wananchi wanaotaabika kutokana na machafuko yanayoendelea huko Syria.

Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa UN Mark Lyall Grant ambaye alikuwa Rais wa Kikao hicho amesema wao wanaendelea kusitikishwa kutokana na serikali ya Syria kuendelea kuwa kikwazo cha misaada kuweza kuwafikia wananchi walioathiriwa.

Licha ya kusikitishwa na kile kinachoendelea lakini Baraza la Usalama kwa kauli moja limelaani kitendo cha serikali ya Syria kukataa kumpa kibali cha kuingia nchini humo Mkuu wa Tume ya Misaada wa Umoja huo Valerie Amos.

Marekani kupitia Msemaji wake wa Wizara ya Mambo ya Nje Victoria Nuland imesema imeridhishwa na hatua ya serikali ya Syria kuwa tayari kuruhusu misaada kuweza kuwafikia wananchi huko Baba Amr.
 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.