Pata taarifa kuu
SYRIA-URUSI

Urusi yavunja ukimya na kupendekeza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kuchukua hatua dhidi ya serikali ya Syria kumaliza mauaji

Urusi kwa mara ya kwanza imeamua kuitisha Mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kwa ajili ya kujadili pendekezo lake jipya la kutaka kuchukuliwa hatua dhidi ya serikali ya Syria.

REUTERS/Omar Ibrahim
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huu wa kushtua umetangazwa na Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa UN Vitaly Churkin ambaye amesema msimamo wa nchi yake kwa sasa ni kutaka kuzuiliwa kuingizwa kwa silaha katika nchi ya Syria.

Balozi Churkin amesema hatua nyingine ambayo inapaswa kuchukuliwa dhidi ya Syria ni kutengwa na Jumuiya ya Kimataifa badala ya kupeleka majeshi kama ambavyo mataifa mengine yamekuwa yakipendekeza.

Hii inakuwa ni mara ya kwanza kwa Urusi kuitaka nchi ya Syria ichukuliwe hatua kama hizo licha ya hapo awali kuwa mpinzani mkubwa wa kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa UN kwa ajili ya kudhibiti mauaji.

Urusi na China zimekuwa mstari wa mbele kukataa hatua zozote za kijeshi dhidi ya Utawala wa Rais Bashar Al Assad licha ya wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kupendekeza hivyo.

Tamko hilo limepokelewa kwa furaha na Ufaransa pamoja na Uingereza ambazo kwa pamoja zimesema huu ni wakati muafaka wa kukubaliana na ukweli wa kile ambacho kinatendeka katika taifa la Syria.

Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa UN Gerald Araud ametoa wito kwa mataifa mengine kutopingana na ukweli wa kile ambacho kinafanywa na serikali ya Rais Bashar Al Assad dhidi ya waandamanaji.

Naye Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa UN Mark Lyall Grant amesema matarajio yake kuona muafaka unapatika juu ya mgogoro unaoendelea katika nchi ya Syria na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha.

Takwimu za Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa UN zinaonesha kuwa watu zaidi ya elfu tano wamepoteza maisha tangu kuzuka kwa mgogoro nchini Syria ambao umedumu kwa karibu miezi kumi sasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.