Pata taarifa kuu
LIBYA

Kiongozi wa Libya atangaza Tume Maalum kuchunguza kifo cha Kanali Gaddafi

Kiongozi wa muda wa nchi ya Libya ambayo imejitangazia ukombozi wake baada ya kifo cha Kanali Muammar Gaddafi ambaye alitawala kwa zaidi ya miongo minne Mustafa Abdel Jalil amesema Tume Maalum ya Uchunguzi ndiyo itasaka ukweli juu ya kifo cha kiongozi huyo kilichotokea alhamisi iliyopita katika Jiji la Sirte.

REUTERS/Suhaib Salem
Matangazo ya kibiashara

Jalil amesema hatua hiyo inakuja baada ya Jumuiya ya Kimataifa pamoja na Mashirika ya Kutetea Haki za Binadamu Duniani kuhitaji majibu ya namna ambavyo Kanali Gaddafi alivyouawa na wapiganaji wa Baraza la Mpito la Taifa la Libya NTC.

Kiongozi huyo wa NTC amekiri ni kweli wananchi wa Libya walikuwa na hamu ya kuona Kanali Gaddafi anafikishwa kwenye Vyombo vya Sheria ili aweze kujibu dhulma ambayo aliifanya dhidi ya wananchi pamoja na ufujaji za mali za taifa hilo.

Jalil ameongeza kuwa wananchi huru wa Libya walitaka kushuhudia Kanali Gaddafi akihukumiwa kifungo na kuishi jela kwa muda mrefu ikiwa kama mshahara wa kile ambacho aliktenda wakati wa utawala wake.

Hatua hii ya kuachiwa jukumu la uchunguzi kwa Tume hiyo maalum linakuja wakati huu ambapo bado mwili wa Kanali Muammar Gaddafi ikiendelea kuanikwa ni wananchi wa Misrata wakipata nafasi ya kuuangalia.

Familia ya Kanali Gaddafi kupitia mwanasheria wa mtoto wake Saadi Gaddafi umeitaka NTC kuwapatia mwili wa baba yake ili waweze kufanya mazishi kwa kufuata taratibu zote za Kiislam badala ya kuendelea kuuanika.

Saadi amesema kile ambacho kinafanywa na NTC kwa sasa ukatili mkubwa zaidi ambao umewahi kuonekana na kama Baba yake alikuwa na makosa ni heri angefikishwa Mahakamani kujibu mashtaka na si kumuua.

Kanali Gaddafi pamoja na mtoto wake Motassim waliuawa kwenye Jiji la Sirte na Majeshi ya NTC ambapo yanatajwa kuongezewa nguvu na mashambulizi yaliyofanywa na Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO.

Kwa sasa vituo vya televisheni vimeanza kuonesha vipande vya video ambavyo vinaonesha jinsi Kanali Gaddafi na Motassim walivyouawa baada ya kukamatwa wakiwa hai huku wauaji wakijigamba kutekeleza tukio hilo.

Nchi ya Libya chini ya Utawala wa NTC hapo jumapili ulitangaza Ukombozi wa Taifa hilo baada ya kifo cha Kanali Gaddafi kilichokuja miezi tisa tangu kuanza kwa mapambano baina ya wafuasi wake na wapiganaji wa utawala huo wakiungwa mkono na Majeshi ya NATO.

Katika hatua nyingine Kiongozi wa Libya Jalil amesema nchi hiyo itakuwa ikiongozwa na sheria za kiislam kama ambavyo ilivyo kwa baadhi ya nchi zilizopo Kaskazini mwa Afrika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.