Pata taarifa kuu
LIBYA-UFARANSA

Kanali Muammar Gaddafi ajiapiza kuendelea kupigana vita kutetea nchi yake

Kiongozi wa Libya ambaye aanakabiliwa na shinikizo la kutakiwa kuondolewa madarakani Kanali Muammar Gaddafi ametoa ujumbe wake wa kwanza tangu akimbilie mafichoni na kujiapiza kuendelea kupigana ili kurejesha nchi hiyo mikononi mwake.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye ujumbe wake ambao umerekodiwa maneno pekee Kanali Gaddafi amewataka wale wote ambao wanapambana naye kujiandaa kwa vita ambayo itakuwa ni ya muda mrefu na kuchangia vifo vya watu wengi zaidi.

Kanali Gaddafi amesema lengo la vita hivi ni kuwaua maadui zake wote wawe wananchi wa Libya na hata wale wakigeni ambao wamekuwa mstari wa mbele kutaka kuuangusha utawala uliopo madarakani.

Kiongozi huyo ambaye amekaa madarakani kwa kipindi cha miaka 42 amesema hawapo tayari kushuhudia mafuta na bandari zinamilikiwa na mataifa ya Magharibi na hivyo watazidisha juhudi kukabiliana na wapinzani wao.

Kanali Gaddafi ambaye hajulikani alipo kwa sasa baada ya baadhi ya watoto zake na mkewe kukimbilia nchini Algeria amewataka wanajeshi wake watiifu kuhakikisha hawarudi nyuma kwa kuwa wao si wanawake ambao watakuwa waoga.

Kauli ya Kanali Gaddafi inarandana na ile ambayo ilitolewa na mtoto wake Seif Al Islam ambaye alisema wanajeshi wao wataendelea kupigana hadi tone la mwisho la damu ili kulitetea taifa lao.

Hapo jana Viongozi wa Dunia ambao walikutana kwenye Mkutano wa Marafiki wa Libya ametangaza kutoa kitita cha $15 bilioni kwa ajili ya kuisadia nchi hiyo katika kipindi hiki cha kuijenga upya.

Uingereza na Ufaransa ambao ndiyo walikuwa waandaaji wa Mkutano huo wamesema licha ya dalili kuonesha Waasi wamepiga hatua na kuweza kuusambaratisha utawala wa Kanali Gaddafi lakini bado kuna kazi ya ziada kuweka utulivu.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron akatumia fursa ya mkutano huo kuweka bayana juhudi ambazo zimefanyika kuuangusha utawala wa Kanali Gaddafi ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Libya kupata mustakabali wake.

Naye mwenyeji wa mkutano huo Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amekiri kuwa wanafanya kila wawezalo katika kuhakikisha majaliwa ya Libya yanapatikana na kuweza kuwa na ustawi bora wa maendeleo.

Katika hatua nyingine licha ya Umoja wa Afrika AU kualikwa kwenye Mkutano huo na kuwakilisha na Jean Ping imeweka bayana kuwa haiutambui utawala wa Baraza la Mpito la Waasi.

Ping amesema msimamo ambao ulitolewa kwenye Mkutano wa mwisho wa AU ulisema unapingana na Majeshi ya Kujihami ya Nchi za Magharibi NATO ulivyofanya mashambulizi na kuwasaidia waasi kusonga mbele.

Vita nchini Libya ambayo ilichangizwa na mapinduzi katika nchi za Tunisia kwa kuangushwa kwa Rais Zine El Abidine Ben Ali na Misri ambapo Utawala wa Rais Hosni Mubarak uling'olewa imedumu kwa zaidi ya miezi sita na kushuhudia maelfu ya watu wakipoteza maisha

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.