Pata taarifa kuu

DRC: Wapinzani waitisha maandamano kupinga uchaguzi wa Desemba

Wagombea watatu wa upinzani waliopigwa mweleka na Rais anayemaliza muda wake Félix Tshisekedi katika uchaguzi wa Desemba 20 walitoa wito siku ya Alhamisi kwa Wakongo kuandamana kuonyesha "kutoridhika" kwao siku ya Jumamosi, siku ya kuapishwa kwa rais, kupinga kile wanachoeleza kama "wizi wa uchaguzi".

Mwanamume aliyekamatwa na maafisa wa polisi wakati wa maandamano huko Kinshasa mnamo Desemba 27, 2023.
Mwanamume aliyekamatwa na maafisa wa polisi wakati wa maandamano huko Kinshasa mnamo Desemba 27, 2023. AFP - JOHN WESSELS
Matangazo ya kibiashara

 

Wapinzani hao ambao ni Moïse Katumbi, Martin Fayulu na Floribert Anzuluni, hata hivyo, hawakuitisha mikusanyiko wala maandamano, bali waliomba "kila mtu popote alipo, aonyeshe kutoridhika kwake, asimame na kusema hapana". Maandamano yalikuwa yamepangwa mnamo Desemba 27 huko Kinshasa na upinzani, lakini yalipigwa marufuku na mamlaka na kusambaratishwa na polisi.

"Tumesitisha vitendo vya watu wengi (...) Hatuwezi kutuma watu kuuawa," amesema Martin Fayulu, ambaye alipata takriban 5% ya kura katika uchaguzi wa urais wa mwezi wa Desemba. Moïse Katumbi, gavana wa zamani wa Katanga (kusini-mashariki), alipata 18% ya kura. Floribert Anzuluni, kama wagombea wengine ishirini, hakufikisha 1% ya kura, huku Félix Tshisekedi, rais tangu mwezi wa Januari 2019 na mgombea wa muhula wa pili, alizidisha 73%, wakati wa uchaguzi wa duru tu. Ataapishwa siku ya Jumamosi katika uwanja mkubwa zaidi wa michezo mjini Kinshasa.

Mwanamke akikimbia na maafisa wa polisi huku mawe yakirushwa wakati wa maandamano ya upinzani mjini Kinshasa mnamo Desemba 27, 2023.
Mwanamke akikimbia na maafisa wa polisi huku mawe yakirushwa wakati wa maandamano ya upinzani mjini Kinshasa mnamo Desemba 27, 2023. AFP - JOHN WESSELS

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Katumbi, Fayulu na Anzuluni wamesisitiza wito wao siku ya Alhamisi wa kufutwa kwa uchaguzi huo ambao wanabaini kwamba uligubikwa na udanganyifu mkubwa. "Wakongo wote wameelewa kuwa ni mchezo wa kuigiza, tumekuwa kicheko cha dunia," amesema Martin Fayulu.

Uchaguzi wa urais ulifanyika wakati huo huo na uchaguzi wa wabunge, wa mikoa na uchaguzi wa madiwani, chaguzi nne ambazo zilianza kama ilivyopangwa Desemba 20 lakini, zilikabiliwa na matatizo mengi ya vifaa, na kufanyika kwa siku kadhaa. Matokeo ya uchaguzi wa urais yalitangazwa Desemba 31 na tume ya uchaguzi (CENI) na kuthibitishwa Januari 9 na Mahakama ya Kikatiba. Matokeo ya muda ya uchaguzi wa wabunge yalitangazwa Januari 14 na CENI na pia yalizua maandamano mengi, hata katika kambi ya rais.

Mnamo Desemba 24, katika misa yake ya Krismasi, askofu mkuu wa Kanisa Katoliki mjini Kinshasa alielezea uchaguzi huo kama "machafuko makubwa yaliyopangwa". Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, maaskofu wa Baraza Kuu la Maaskofu nchini DRC Kongo (CENCO) wamezungumza juu ya "janga la uchaguzi" lakini, huku wakiomba mahakama "kubatilisha walioidhinisha uongo", na kutoa wito kwa raia "kufanya mazungumzo, utulivu, amani na kujizuia na vurugu za kila aina".

Mmoja wa waandamanaji wakati wa maandamano ya upinzani mjini Kinshasa mnamo Desemba 27, 2023.
Mmoja wa waandamanaji wakati wa maandamano ya upinzani mjini Kinshasa mnamo Desemba 27, 2023. AFP - JOHN WESSELS
Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.