Pata taarifa kuu
USHIRIKIANO-DIPLOMASIA

Burkina Faso na Urusi zasaini mkataba wa ujenzi wa kinu cha nyuklia

Burkina Faso na Urusi zinaendelea kuimarisha uhusiano wao: nchi hizi mbili zimetia saini kwenye makubaliano ya ujenzi wa kinu cha nyuklia katika nchi hii ya Sahel ambapo chini ya robo ya wakazi wana umeme.

Rais wa Burkina Faso Ibrahim Traore, kushoto, na Rais wa Urusi Vladimir Putin wakipeana mikono kabla ya sherehe rasmi ya kuwakaribisha viongozi kwenye Mkutano wa Wakuu wa Urusi na Afrika huko St. Petersburg, Urusi, Julai 27, 2023.
Rais wa Burkina Faso Ibrahim Traore, kushoto, na Rais wa Urusi Vladimir Putin wakipeana mikono kabla ya sherehe rasmi ya kuwakaribisha viongozi kwenye Mkutano wa Wakuu wa Urusi na Afrika huko St. Petersburg, Urusi, Julai 27, 2023. AP - Sergei Bobylev
Matangazo ya kibiashara

Burkina Faso, inayoongozwa na utawala wa kijeshi tangu mwaka jana, inatafuta kuwageukia washirika wake wapya na imejisogeza karibu na Urusi.

"Serikali ya Burkina Faso imetia saini mkataba wa maelewano wa ujenzi wa kinu cha nyuklia," imebainishwa kwenye taarifa kwa vyombo vya habari. "Ujenzi wa kinu hiki cha nyuklia unalenga kufidia mahitaji ya nishati ya raia," taarifa hiyo imeongeza.

Kusainiwa kwa makubaliano haya kulifanyika katika hafla ya Wiki maksusi ya Nishati ya Urusi ambayo imefanyika huko Moscow, ambapo Waziri wa Nishati wa Burkina, Simon-Pierre Boussim, alishiriki. Kwa upande wa Urusi, hati hiyo imetiwa saini na Nikolay Spasski, naibu mkurugenzi mkuu wa shirika la nyuklia la Rosatom.

"Mkataba huo unajumuisha waraka wa kwanza katika sekta ya matumizi ya amani ya nishati ya atomiki kati ya Urusi na Burkina Faso," Rosatom imesema katika taarifa yake.

Hati hiyo "inakuja kutimiza matakwa ya rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, yaliyotolewa mwezi Julai mwaka huu wakati wa mkutano wa kilele wa Urusi na Afrika wakati wa mazungumzo na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin", inaeleza serikali ya Burkina Faso.

Mwishoni mwa mwaka 2020, ni 22.5% tu ya raia wa Burkina Faso (67.4% katika maeneo ya mijini, 5.3% katika maeneo ya vijijini) walikuwa na umeme, kulingana na takwimu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

"Tunapanga, kama tunaweza, kujenga vinu vya nyuklia ifikapo 2030, ili kutatua tatizo la upungufu wa nishati," Waziri Boussim alitangaza siku ya Alhamisi, akinukuliwa na shirika la habari la Urusi la TASS. "Changamoto yetu ni kuongeza uzalishaji wetu wa umeme maradufu ifikapo mwaka 2030, jambo ambalo litatuwezesha kuinua ukuaji wa viwanda barani Afrika," aliongeza.

Burkina Faso inaagiza sehemu kubwa ya umeme wake kutoka nchi jirani za Côte d'Ivoire na Ghana na inazalisha sehemu nyingine ndani ya nchi, hasa kwa umeme wa maji au nishati ya jua. Bara la Afrika kwa sasa lina kinu kimoja tu cha nyuklia, nchini Afrika Kusini huko Koeberg, karibu na Cape Town.

Burkina Faso inatawaliwa na Kapteni Ibrahim Traoré, ambaye aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya Septemba 2022, ya pili katika kipindi cha miezi minane. Tangu kuingia madarakani, Burkina imejitenga na Ufaransa, mshirika wa kihistoria na ambayo iliitawala katika enzi za ukoloni, hasa kwa kuitaka kuwaondoa wanajeshi wake nchini Burkina Faso mwezi Februari.

Katika kutafuta washirika wapya, Ouagadougou imesogelea Moscow. Vladimir Putin alitangaza wakati wa mkutano wa kilele wa Saint Petersburg mwezi Julai kwamba Moscow itapeleka nafaka bila malipo kwa nchi sita za Afrika, ikiwa ni pamoja na Burkina Faso, katika miezi ijayo.

Mwanzoni mwa Septemba, ujumbe wa Urusi ukiongozwa na Naibu Waziri wa Ulinzi, Yunus-Bek Yevkurov, ulikwenda Ouagadougou kujadili masuala ya maendeleo na ushirikiano wa kijeshi na Ibrahim Traoré. Mnamo Septemba 30, katika mahojiano kwenye televisheni ya taifa, Kapteni Traoré alithibitisha kwamba vifaa vingi vya jeshi la Burkina Faso vilikuwa vya Kirusi.

Burkina Faso imekuwa ikikabiliwa na machafuko mabaya na ya mara kwa mara ya wanajihadi katika sehemu kubwa ya ardhi yake kwa miaka kadhaa, ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 17,000 na zaidi ya milioni mbili wakimbizi wa ndani. Burkina Faso imeunda muungano na Mali na Niger, nchi mbili zinazoongozwa na tawala za kijeshi ambazo pia zinadumisha uhusiano mzuri na Moscow, ndani ya mfumo wa Muungano wa Nchi za Sahel (AES), ushirikiano wa kiulinzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.