Pata taarifa kuu
USHIRIKIANO-DIPLOMASIA

Mapinduzi yakithiri Afrika: EU yataka 'mbinu mpya ya kimkakati' na Afrika

Umoja wa Ulaya unataka kufafanua mbinu mpya ya kimkakati kwa Afrika inayolenga ushirikiano na "serikali halali", baada ya mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi na kutokana na ushawishi wa Urusi, amesema rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen leo Jumatano Septemba 13, 2023.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen akitoa hotuba yake ya kila mwaka ya Hali ya Umoja wa Ulaya kwa Bunge la Ulaya Jumatano Septemba 13, 2023 mjini Strasbourg.
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen akitoa hotuba yake ya kila mwaka ya Hali ya Umoja wa Ulaya kwa Bunge la Ulaya Jumatano Septemba 13, 2023 mjini Strasbourg. AP - Jean-Francois Badias
Matangazo ya kibiashara

"Lazima tuonyeshe, kuhusiana na Afrika, umoja wa nia ambayo tumeonyesha kuhusu Ukraine," Bi. von der Leyen amewaambia wabunge, akiwa na wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mamlaka ya Urusi barani Afrika, na hasa katika kanda ya Sahel. "Urusi inashawishi na kunufaika kutokana na machafuko katika kanda ya Sahel," ameongeza katika hotuba yake kuhusiana na Muungano.

Kutokana na hali hii, "lazima tuzingatie ushirikiano na serikali halali na mashirika ya kikanda," amesisitiza. Tangu mwaka 2020, Mali, Chad, Burkina Faso na Niger zimekumbwa na mapinduzi ya kijeshi, ambayo "yatachangia kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu katika eneo hilo katika miaka ijayo," amelalamika. Mwishoni mwa mwezi Agosti, nchi nyingine ya Afrika, Gabon, iliongezwa kwenye orodha hiyo.

Mbinu hii mpya ya kimkakati lazima ifafanuliwe kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kilele kati ya Umojawa Ulaya na Umoja wa Afrika, uliopangwa kufanyika 2025, ameongeza. Siku moja kabla, mkuu wa diplomasia ya Ulaya Josep Borrell alikuwa ametambua kushindwa kwa nchi za Ulaya kuimarisha demokrasia katika kanda ya Sahel, licha ya kuwekeza mamia ya mamilioni ya euro, ambayo hayakuzuia mapinduzi ya kijeshi.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Umoja wa Ulaya umetumia euro milioni 600 kwa misheni ya kiraia na kijeshi katika kanda ya Sahel, na kutoa mafunzo kwa makumi ya maelfu ya askari polisi na wanajeshi nchini Mali na Niger, Bw. Borrell alisema wakati wa mjadala katika Bunge la Ulaya huko Strasbourg. "Hii haikusaidia kuimarisha vikosi vya kijeshi vinavyounga mkono serikali ya kidemokrasia", bali vikosi vya jeshi "ambavyo vinaiangusha", hata hivyo amekiri.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.