Hali ya utulivu yaanza kushuhudiwa Amhara Ethiopia
Jimbo la Amhara nchini Ethiopia, limeanza kushuhudia utulivu wakaazi wakisema ni kutokana na jeshi la taifa kuwazidi nguvu wapiganaji wa eneo hilo na kuchukuwa udhibiti wa baadhi ya miji baada ya mapigano ya siku kadhaa.
Imechapishwa:
Idara ya hali ya dharura nchini humo imesema jeshi la taifa limefanikiwa kukomboa jimbo la Amhara baada ya watu wenye silaha inaowaita magaidi kuzidiwa nguvu.
Ni taarifa ambayo pia wafanyakazi wa kutoa misaada eneo hilo wamesema miji mingi ambayo imekuwa ikikaliwa na wapiganaji sasa inathibitiwa na wanajeshi wa serikali, licha ya kwamba bado baadhi inakaliwa na wapiganaji hao wa Fano.
Hakuna taarifa rasmi iliotolewa na mamlaka za Ethiopia kuhusu hali ya eneo la Amhara ila madaktari eneo hilo wamekiri kupokea miili ya raia kadhaa ambao wameuawa kutokana na makabiliano kati ya jeshi wa wapiganaji wa Fano.
Serikali ya Ethiopia jumatano ilitangaza hali ya dharura katika jimbo hilo la Amhara ambalo limekuwa lishuhudia utovu wa usalama.