Pata taarifa kuu

Ramaphosa kuongoza marais wa Afrika kupatanisha Urusi na Ukraine Ijumaa

NAIROBI – Viongozi wa mataifa manne ya Afrika, wakiongozwa na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wanaelekea nchini Ukraine na Urusi siku ya Ijumaa, kuzungumza na viongozi wa nchi hizo mbili kuhusu vita vinavyoendelea.  

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akihudhuria Kongamano la Kilele la Kazi Duniani katika Palais des Nations huko Geneva, Uswizi Juni 14, 2023.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akihudhuria Kongamano la Kilele la Kazi Duniani katika Palais des Nations huko Geneva, Uswizi Juni 14, 2023. © @PresidencyZA
Matangazo ya kibiashara

Baada ya kuwasili jijini Kiev, marais hao wa Afrika watakutana na rais Volodymyr Zelensky kabla ya kuelekea jijini Saint Petersburg kukutana na rais Vladmir Putin.  

Awali, safari hii ilikuwa iwashirikishe marais saba, lakini rais wa Uganda Yoweri Museveni anaumwa, baada ya kuambukizwa virusi vya Uviko 19, rais wa Misri Abdel Al-Sisi hajathibitisha ushiriki wake lakini Denis Sassou Nguesso, yeye alijiondoa baada ya kutaka safari hiyo kuahirishwa kwa sababu za kiusalama.  

Katika ziara hiyo, rais Ramaphosa ataungana na mwenzake wa Senegal Macky Sall, Hakainde Hichilema kutoka Zambia na Azali Assoumani, rais wa Comoro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.  

Ziara hii inakuja, baada ya miezi kadhaa iliyopita rais Ramaphosa kutangaza kuwepo kwa mpango kwa viongozi wa Afrika kujaribu kusuluhisha mzozo kati ya Urusi na Ukraine.  

Aidha, ziara hii imetanguliwa na ziara ya mawaziri wa Mambo ya nje kutoka Urusi na Ukraine katika baadhi ya mataifa ya Afrika, kuomba uungwaji mkono kuhusu vita vinavyoendelea. Mataifa mengi ya Afrika yanasema hayaegemei upande wowowte kwenye vita hivyo.  

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, umeathiri mataifa ya Afrika kwa kusababisha kupanda kwa gharama ya maisha, kutokana na uhaba wa nafaka hasa ngano inayotegemewa sana barani Afrika.  

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.