Burkina Faso: Daktari wa Australia aachiliwa miaka 7 baada ya kutekwa nyara
Daktari wa Australia mwenye umri wa miaka 88, Kenneth Elliott, ameachiliwa miaka saba baada ya kutekwa nyara na wanajihadi nchini Burkina Faso, serikali ya Australia imetangaza Ijumaa.
Imechapishwa:
Kenneth Elliott na mkewe walitekwa nyara na wanajihadi wenye uhusiano na Al-Qaeda mnamo Januari 2016. Mkewe Jocelyn aliachiliwa mwezi uliofuata.
Daktari huyo wa upasuaji alirejea Australia Alhamisi jioni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong amewaambia waandishi wa habari.
“Daktari Elliott yuko salama na ameungana tena na mkewe Jocelyn na watoto wao,” Bi Wong amesema.
"Nina furaha kubwa kwamba kuachiliwa kwake kumepatikana na kwamba yuko salama tena na familia yake," ameongeza.
Kutekwa nyara kwa wanandoa hao kulidaiwa na kundi la wanajihadi la Ansar Dine, linalohusishwa na Al-Qaeda.
Mnamo Julai 2017, shirika la Al-Qaeda huko Maghreb (Aqmi) lilirusha video inayoonyesha mateka sita, akiwemo Kenneth Elliott.