Hali ilivyo nchini Sudan kufikia leo Jumanne
NAIROBI – Pande zinazopigana nchini Sudan, zimekubaliana kuhusu hatua ya kusitishwa kwa makabiliano katika kipindi cha saa 72, hatua inayokuja wakati huu mataifa ya Magahribi, nchi za kiarabu na Asia yakiwemo mataifa mengine ya Afrika yakiendelea kuwaondoa raia wake nchini humo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Licha ya makubaliano hayo, kumeripotiwa kuzuka kwa makabiliano katika eneo la Geneina Magharibi mwa jimbo la Darfur kati ya wanajeshi wa Sudan na wanajeshi maalum wa RSF.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa mapigano yanyoendelea nchini humo yanaweza kuathiri mataifa jirani na taifa hilo.
Raia na majeruhi
Karibia watu zaidi ya 427 wamethibitishwa kufariki katika mapigano hayo wakati wengine zaidi ya 3,700 wakiwa wamejeruhiwa kwa mujibu wa ripoti ya umoja wa mataifa.
Makumi kwa maelfu ya watu, wakiwemo raia wa Sudan na raia wa kigeni, wamekimbilia nchini Misri, Chad na Sudan Kusini katika siku chache zilizopita.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kuna uhaba mkubwa wa chakula, maji safi, dawa na mafuta na uhaba wa mawasiliano na umeme. Bei za bidhaa hizo pia zikiripotiwa kupanda.
Diplomasia
Jeshi la Sudan na RSF wamekubaliana kusitisha mapigano kwa saa 72 baada ya kufanyika kwa mazungumzo ya kina, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema muda mfupi kabla ya kutekelezwa kwa makubaliano hayo kuanzia saa sita usiku wa kuamkia leo Jumanne.
"Usitishaji huu wa mapigano unalenga kuruhusu raia na wakaazi kupata rasilimali muhimu, huduma za afya, na maeneo salama, huku pia wakiwaondoa raia wa kigeni kwa kuzingatia kidiplomasia," RSF iliandika kwenye Twitter.
Blinken alisema Marekani itaratibu na maslahi ya kiraia ya kikanda, kimataifa na Sudan kuunda kamati ya kusimamia kazi ya usitishaji vita wa kudumu na mipango ya kibinadamu.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa linapanga mkutano kuhusu Sudan siku ya Jumanne.
Mataifa kadhaa - ikiwa ni pamoja na Kanada, Ufaransa, Poland, Uswizi na Marekani - yamesitisha shughuli katika balozi zake katika kipindi cha muda usiojulikana.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa aliwataka wanachama 15 wa baraza la usalama kutumia nguvu zao kuirejesha Sudan katika njia ya mpito ya kidemokrasia.