Makabiliano yanaendelea nchini Sudan, mataifa ya kigeni yakiwaondoa raia wake
NAIROBI – Mapigano yameingia wiki ya pili leo nchini Sudan, kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo wa RSF, ambayo yamesababisha watu zaidi ya 400 kupoteza maisha na maelfu kujeruhiwa.
Imechapishwa:
Wakaazi wa Khartoum, wameendelea kusikia, milio ya risasi na milipuko, baada ya utulivu wa muda mfupi kushuhudiwa hapo jana, siku ya kwanza ya Sikukuu ya Eid.
Licha ya pande zote kukubali kuacha mapigani wakati wa sikukuu ya Eid, wakabiliano yameendelea, huku jeshi la Sudan likitangaza kuwa limekubali kusaidia mipango ya kuwaondoa nchini humo raia wa kigeni.
Saudi Arabia imekuwa nchi ya kwanza kufanikiwa kuwaondoa raioa wake 50 baada ya kutumia usafiri wa boti ambao wamewasili kwenye mji wa bandari wa Jeddah.
Wachambuzi wa mizozo kutoka Shirika la International Crisis Group, wanaonya kuwa iwapo suluhu ya haraka haitapatikana, huenda ukasambaa na kuwa wa kikanda.
Haya yanajiri wakati huu jeshi la Sudan likisema kuwa wanadiplomasia na raia kutoka katika nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa na China wataondolewa nchini humo kwa ndege wakati huu huku mapigano yakiendelea kati ya wanajeshi wa serikali na vikosi maalum vya RSF.
Saudi Arabia pia imetangaza kuwa inapanga kuwahamisha raia wa Saudia na raia wa nchi "ndugu" kutoka Sudan.
Jeshi la Sudan limesema kuwa tume ya kidiplomasia ya Saudi Arabia tayari imeondolewa. Mgogoro huo umeingia wiki yake ya pili licha ya pande zote mbili - jeshi na RSF kukubaliana kusitisha mapigano kwa siku tatu kuadhimisha sikukuu ya Waislamu ya Eid al-Fitr.