Pata taarifa kuu
USALAMA-UGAIDI

Nigeria: Wanajeshi watatu wauawa katika mlipuko wa bomu la kutegwa ardhini

Wanajeshi watatu waliuawa siku ya Alhamisi na watu 11, wakiwemo raia saba, walijeruhiwa katika mlipuko wa bomu la kutegwa ardhini kaskazini mashariki mwa Nigeria, eneo linalokabiliwa na mashambulizi ya waasi wa kijihadi, wanamgambo wawili na mtu mmoja wameliambia shirika la habari AFP siku ya Ijumaa.

Katika siku za nyuma, ISWAP na mpinzani wake Boko Haram wameanzisha mashambulizi kadhaa ndani na karibu na Banki, yakilenga wanajeshi na watu waliokimbia makazi yao.
Katika siku za nyuma, ISWAP na mpinzani wake Boko Haram wameanzisha mashambulizi kadhaa ndani na karibu na Banki, yakilenga wanajeshi na watu waliokimbia makazi yao. AP - Chinedu Asadu
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Alhamisi jioni, gari la askari waliokuwa wakipiga doria lilikanyaga bomu la kutegwa ardhini kwenye barabara kuu kilomita 10 kutoka mji wa Banki, katika Jimbo la Borno, karibu na mpaka na Cameroon, na kuua wanajeshi watatu na kuwajeruhi vibaya wengine wanne, duru zimesema.

Lori lililokuwa limewabeba wakaazi wa mji mkuu wa mkoa Maiduguri kuelekea Banki kwa uchaguzi wa ugavana siku ya Jumamosi pia lilikanyaga bomu la kutegwa ardhini na abiria saba walijeruhiwa, vyanzo hivyo vimesema.

"Wanajeshi watatu walikufa katika mlipuko huo na wengine wanne walijeruhiwa vibaya, huku raia saba pia wakijeruhiwa," amesema Usman Hamza, mwanachama wa wanamgambo wanaopinga wanajihadi. Afisa wa kijeshi na mwanamgambo mwingine kwa sharti la kutotajwa jina amethibitisha idadi hiyo. Jeshi halikusema chochote kuhusiana na mlipuko huo.

Bw. Hamza alishutumu kundi la wanajihadi la Islamic State katika Afrika Magharibi (ISWAP), linaloendesha uhalifu wake katika eneo hilo, kwa kutega mabomu. Katika siku za nyuma, ISWAP na mpinzani wake Boko Haram wameanzisha mashambulizi kadhaa ndani na karibu na Banki, yakilenga wanajeshi na watu waliokimbia makazi yao.

Mji huo una takriban watu 45,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo wa wanajihadi ambao umedumu kwa miaka 14 na ambao umesababisha vifo vya watu 40,000 na milioni mbili kukimbia makazi yao kulingana na Umoja wa Mataifa. Ghasia hizo zimeenea hadi nchi jirani za Niger, Chad na Cameroon, na kusababisha kuundwa kwa muungano wa kijeshi wa kikanda ili kupambana na makundi ya kijihadi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.