Pata taarifa kuu
HAKI ZA BINADAMU

Rais Museveni atetea uamuzi wa kuifunga ofisi ya haki ya Umoja wa Mataifa

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametetea uamuzi wa serikali yake wa kusitisha operesheni za ofisi za tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binadamu nchini Uganda OHCHR.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni © StateHouseUganda
Matangazo ya kibiashara

Kauli hiyo ameitoa baada ya mwanahabari mmoja kuhoji hatua ya kufungwa kwa operesheni za tume hiyo, wakati wa kikao na wanahabari siku ya Jumatano nchini Afrika Kusini, kwenye mkutano wa uwekezaji kati ya Uganda na Afrika kusini.

Hii ni kwa sababu tuna tume ya haki za kibinadamu nchini Uganda, ambayo ina mamlaka kikatiba, kwa hivyo kuwa na nyingine ambazo hazina mamlaka kikatiba, kwanza sio muhimu na pili ni kupindisha mambo, kwa sababu baadhi ya watu wanaweza wasijue tofauti. Amesema Museveni.

Katika kauli yake ambayo ilipeperushwa na televisheni ya kitaifa ya serikali ya Afrika Kusini SABC, rais Museveni ameongeza kuwa badala ya watu kuenda kuripoti sehemu ambayo hatua zinaweza kuchukuliwa wanaenda Umoja wa Mataifa ambayo haina mamlaka.

Mwanzoni mwa mwezi Februari, 2023, Uganda kupitia barua kutoka wizara ya mambo ya nje kwa tume hiyo, ilisema haitaiongezea muda tume hiyo kuendelea kuhudumu nchini Uganda, kwa kigezo kuwa nchi hiyo sasa ina uwezo wa kufuatilia, kukuza na kulinda haki za binadamu bila msaada kutoka nje.

Serikali kukosolewa

Kwa miaka mingi sasa, upinzani, wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na  mataifa ya magharibi, wamekuwa wakiikashifu serikali ya Museveni, kwa ukiukaji mbalimbali wa haki, ikiwemo mateso, kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, mauaji ya wapinzani na wakosoaji, na pia kukamatwa tena kwa watu walioachiliwa kisheria na mahakama.

Ni madai ambayo utawala wa Musevei umekuwa ukikanusha, ukisema maofisa wa usalama wote waliohusishwa na ukiukaji huo wameshaadhibiwa.

Ofisi kubuniwa

Kwa mujibu wa serikali ya Uganda, ofisi ya OHCHR nchini Uganda, ilibuniwa mwaka 2006, na hapo awali, ilikubaliwa kuangazia masuala ya haki za binadamu katika maeneo ya migogoro haswa Kaskazini na kaskazini mashariki.

Baadaye ofisi hiyo ilikubaliwa kuangazia masuala ya haki kote nchini.

Ilivyo kwa sasa, baada ya kauli hii ya serikali ya Uganda, muda ya tume hiyo kuendelea kuhudumu nchini humo utakamilika mwishoni mwa mwezi Machi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.