Pata taarifa kuu
DRC - USALAMA

DRC: Waasi watakiwa kuondoka katika maeneo wanayoshikilia kufikia mwezi Machi

Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, waliokutana pembezoni mwa mkutano wa wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika nchini Ethiopia, kujadili hali ya usalama Mashariki mwa DRC, wameyataka makundi yenye silaha kuondoka katika maeneo wanayodhibiti kufikia mwisho wa mwezi Machi.

Ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 18 Februari 2023.
Ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, tarehe 18 Februari 2023. AFP - EDUARDO SOTERAS
Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo uliofanyika jijini Addis Ababa, ulihudhuriwa na viongozi saba wa nchi wanachama, akiwemo rais wa DRC Felix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda.

Jumuiya ya Afrika Mashariki katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa Twitter, imesema, viongozi hao wamekubaliana kuwa makundi ya waasi, likiwemo lile la M 23, yaondoke katika maeneo wanayoshikilia kufikia tarehe 30 mwezi Machi.

Aidha, wametaka makundi hayo ya waasi kuweka silaha chini mara moja na yawache kupigana, na kuongeza kuwa raia waliokimbia makwao, warejeshwa nyumbani.

Kikao hicho kinaelezwa kudumu kwa saa nne, huku ripoti zikisema rais Tshisekedi ametaka jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kutumia nguvu dhidi ya M 23, iwapo hawatajiondoa kwenye maeneo wanayoshikilia.

Rais wa Kenya William Ruto, ambaye nchi yake imechukua uongozi wa kusaidia kuleta amani Mashariki mwa DRC ambako imetuma kikosi chake, amesema uongozi wa kisiasa unahitajika nchini humo kumaliza kuteseka kwa raia, lakini pia akiyataka mataifa ya ukanda kuunganisha nguvu, kuisaidia kuleta amani ya kudumu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mkutano huu umekuja baada ya viongozi hao kukutana jijini Bujumbura nchini Burundi mapema mwezi huu na kutoa wito kama huo, lakini pia wakuu wa majeshi kutoka nchi wanachama kukutana Nairobi na kuwataka waasi wa M 23 kuanza kujiondoa kuanzia tarehe 28 Februari.

Naye katibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress akiwahotubia viongozi hao wa Afrika, amewataka kuchukua hatua kwa ajili ya amani ya kudumu Mashariki mwa DRC na eneo la Sahel.

Siku ya Ijumaa, Guterres, alikutana na rais Paul Kagame kwa ajili ya mazungumzo kuhusu usalama Mashariki mwa DRC.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.