Pata taarifa kuu

Niger: Watu 192 waangamia kutokana na mafuriko

Mvua kubwa ambazo zimekuwa zikinyesha nchini Niger tangu mwezi Juni na mafuriko makubwa yanayosababishwa na mvua hizo yamesababisha vifo vya watu 192 na zaidi ya watu 263,000 kupoteza makazi na mali zao, na kufanya msimu wa mvua wa mwaka huu kuwa mbaya zaidi katika historia ya nchi hiyo.

Mkazi wa wilaya ya Kirkissoye akiangalia nyumba yake iliyoharibiwa na mafuriko huko Niamey, Septemba 3, 2019.
Mkazi wa wilaya ya Kirkissoye akiangalia nyumba yake iliyoharibiwa na mafuriko huko Niamey, Septemba 3, 2019. AFP - BOUREIMA HAMA
Matangazo ya kibiashara

Kufikia Oktoba 4, mafuriko yalikuwa yamesababisha vifo vya watu 192 kote nchini, ikiwa ni pamoja na 136 walioporomokewa na nyumba na watu 56 waliokufa maji baada ya kusombwa na maji, kulingana na takwimu za kitengo cha polisi cha Ulinzi wa raia zilizotolewa kwa shirika la habari la AFP siku ya Alhamisi. Baadhi ya watu 211 walijeruhiwa na wengine 263,671 waliokosa makazi.

Msimu wa mvua unapokaribia kuisha, idadi ya mafuriko imeongezeka kwa wiki kadhaa: ripoti ya mwisho iliyotolewa Septemba 18 iliripoti vifo 159, waathiriwa 225,539 na 185 kujeruhiwa. Mikoa iliyoathiriwa zaidi ni Maradi, katikati-kusini, 74 waliokufa, Zinder, katikati-mashariki, 61 waliokufa, Dosso, kusini-magharibi, 27 waliokufa, na Tahoua, magharibi, 18 wamekufa.

Niamey, mji mkuu wa Niger wenye wakazi milioni mbili, umerekodi vifo viwili na zaidi ya watu 1,300 waliopoteza mali zao, hususan nyumba. Mvua hizo pia zimeharibu kabisa aukusomba nyumba 30,397, madarasa 83, vituo sita vya matibabu na maghala 232 ya nafaka. Karibu ng'ombe 700 pia waliangamizwa.

Mafuriko mabaya zaidi katika miaka kumi

Msimu wa mvua - kati ya mwezi wa Juni na Septemba - mara kwa mara huua watu nchini Niger, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya jangwa la kaskazini, lakini idadi vifo ni kubwa zaidi mwaka huu. Mnamo 2021, watu 70 walikufa na wengine 200,000 walikosa makaazi.

Kwa miezi kadhaa, nchi jirani ya Nigeria pia ilikumbwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kutokea katika muongo mmoja: katika sehemu yake ya kaskazini pekee, zaidi ya watu 300 walifariki, angalau 100,000 walilazimika kukimbia makaazi yao na mazao yaliangamizwa, kulingana na mamlaka.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.