Pata taarifa kuu

Meli iliyobeba ngano ya Ukraine yawasili Djibouti

Meli iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa iliyosheheni tani 23,000 za ngano kutoka Ukraine ikielekea Ethiopia, ambako mamilioni ya watu wamekumbwa na njaa, imewasili katika bandari ya Djibouti siku ya Jumanne, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza.

Meli ya kwanza iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa inapakia zaidi ya tani 23,000 za nafaka kusafirisha hadi Ethiopia, huko Yuzhne, mashariki mwa Odessa kwenye pwani ya Bahari Nyeusi, mnamo Agosti 14, 2022.
Meli ya kwanza iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa inapakia zaidi ya tani 23,000 za nafaka kusafirisha hadi Ethiopia, huko Yuzhne, mashariki mwa Odessa kwenye pwani ya Bahari Nyeusi, mnamo Agosti 14, 2022. AFP - OLEKSANDR GIMANOV
Matangazo ya kibiashara

Meli iitwayo Brave Commander iliondoka kwenye bandari ya Pivdenny nchini Ukraine mnamo Agosti 16, baada ya makubaliano kati ya Kyiv na Moscow yaliyotiwa saini mnamo mwezi Julai, chini ya uangalizi wa Uturuki na Umoja wa Mataifa, kuwezesha usafirishaji wa nafaka za Ukraine zilizozuiwa kwa sababu ya vita kati ya nchi hizo mbili.

"Meli ya kwanza ya WFP iliyobeba nafaka za Ukraine tangu mwezi wa Februari imewasili nchini Djibouti. Sasa tupakua ngano hii na kuituma Ethiopia," mkurugenzi mtendaji wa WFP David Beasley ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Tani hizi 23,000 za ngano "zitatumika kuunga mkono mwitikio wa kibinadamu wa WFP nchini Ethiopia ambako zaidi ya watu milioni 20 wanakabiliwa na njaa", pia WFP katika kanda ya Afrika imesema katika ujumbe mwingine wa Twitter.

Eneo la Kaskazini mwa Ethiopia linakabiliwa na mzozo mkubwa wa kibinadamu, uliosababishwa na mzozo uliodumu tangu mwezi Novemba 2020 kati ya serikali na waasi katika mkoa wa Tigray, wakati maeneo ya kusini na kusini-mashariki mwa nchi hiyo yanakabiliwa na ukame wa kihistoria unaoikumba Pembe ya Afrika, tukio mbaya zaidi tangu miaka 40.

Kulingana na WFP, watu milioni 22 wanatishiwa na njaa katika ukanda mzima, hasa nchini Somalia, Ethiopia na Kenya.

Misimu minne ya kukosekana kwa mvua tangu mwishoni mwa 2020, hali ambayo imeua mamilioni ya mifugo na kuharibu mazao, na Shirika la Hali ya Hewa Duniani la Umoja wa Mataifa lilionya wiki iliyopita juu ya kutonyesha kwa mvua za kutosha katika msimu ujao wa mvua, kati ya mwezo Oktoba na Desemba.

Ukraine na Urusi ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa nafaka duniani, ambao bei yao imepanda tangu kuanza kwa vita.

Kulingana na Kituo cha Uratibu wa Pamoja ambacho kinasimamia ukanda wa bahari unaoruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka bandari za Ukraine, zaidi ya tani 721,000 tayari zimeondoka nchini kwa njia ya bahari.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.