Senegal kuendelea kutoa mchango wake wa kijeshi nchini Mali
Jeshi la Senegal limesema litaendelea kuhudumu katika jeshi la kulinda amani katika nchi jirani ya Mali, baada ya kiongozi wa upinzani kutaka jeshi hilo kurudi nyumbani.
Imechapishwa:
Katika taarifa yake, jeshi limekanusha ripoti kuwa, linapanga kuondoa vikosi vyake vinavyokadiriwa kuwa zaidi ya 1300 nchini Mali, na kusisitiza kuwa kinachofanyika, ni mzunguko wa kawaida.
Senegal ambayo inachangia idadi kubwa katika jeshi ma MINUSMA nchini Mali, imeendelea kuwa miongoni mwa wanajeshi wa kigeni wanaosaidia nchi hiyo kupambana na makundi ya kijihadi.
Ousmane Sonko, mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji mkubwa wa rais Macky Sall, amemtuhumu rais wa nchi hiyo kwa kutuma wanajeshi hao katika nchi hiyo jirani kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa Ufaransa.
Sonko ambaye amesema atawania urais mwaka 2024, anasema iwapo ataingia madarakani, atatuma jeshi la nchi yake kushirikiana na lile la Mali kupambana na wanajihadi na kuliondoa kwenye MINUSMA.
Hii imekuja baada ya Ufaransa kuondoa kabisa wanajeshi wake nchini humo, baada ya kutofautiana na uongozi wa kijeshi.