Aliyekuwa rais wa Somalia amtuhumu rais wa sasa kushambulia makazi yake
Rais wa zamani wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud amesema Jumapili kwamba wanajeshi walishambulia makazi yake na kwamba Rais Mohamed Abdullahi Mohamed ndiye aliyehusika na operesheni hiyo.
Imechapishwa:
Kauli yake inakuja wakati makundi mawili ya wanajeshi walikabiliana kwa kurushiana risasi katika mji mkuu wa Mogadishu, ishara ya kuongezeka kwa mgawanyiko ndani yavikosi vya jeshi na usalama kati ya wafuasi wa rais wa sasa ambao walitaka aongezewe muhula wake na wale wanaopinga.
Kulingana na wadadisi, migawanyiko hii inaweza kuvuruga vikosi vya usalama vya Somalia kutoka kwenye vita vyao dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al Shabaab, lenye mafungamano na al-Qaeda.
Rais Mohamed Abdullahi Mohamed alipitisha sheria katikati ya mwezi wa Aprili kuongeza muhula wake hadi miaka miwili, na kusababisha wimbi la upinzani nchini Somalia na kimataifa. Muhula wake wa miaka minne ulimalizika mwezi wa Februari mwaka huu bila mrithi yeyote kuteuliwa.