Pata taarifa kuu

Nguesso katika jaribio jingine la kuongoza Congo kwa zaidi ya miaka 36

Raia nchini Congo Brazzaville, Jumapili hii watapiga kura kuchagua rais katika uchaguzi ambao umesusiwa na chama kikuu cha upinzani nchini humo.

Rais wa Congo-Brazzaville, Denis Sassou-Nguesso, katika picha ilikuwa tarehe 30/09/2019, jijini Paris, Ufaransa.
Rais wa Congo-Brazzaville, Denis Sassou-Nguesso, katika picha ilikuwa tarehe 30/09/2019, jijini Paris, Ufaransa. AP - Kamil Zihnioglu
Matangazo ya kibiashara

Rais Denis Sassou Nguesso, ambaye ameongoza taifa hilo lenye utajiri wa mafuta na watu zaidi ya milioni 5 kwa zaidi ya miaka 36, anaomba kuchaguliwa tena kwa kipindi cha miaka 5.

Nguesso, ambaye sasa ana umri wa miaka 77, anakabiliwa na upinzani toka kwa wagombea wengine 6, lakini bado anapewa nafasi kubwa ya kushinda.

Kwa mara ya kwanza Nguesso alihudumu kama rais kati ya mwaka 1979 hadi 1992, ambapo alimaliza utawala wake wa mihula mitatu chini ya mfumo wa vyama vingi.

Hata hivyo alichukua tena nchi mwaka 1997 baada ya vita fupi ya wenyewe kwa wenyewe, ambapo waasi wa wakati huo walimuondoa madarakani aliyekuwa rais Pascal Lissouba, na tangu wakati huo amekuwa madarakani.

Alichaguliwa tena mwaka 2002 na kwa mara nyingine tena mwaka 2009, ambapo iliaminika kuwa muhula wake wa mwisho wa miaka 7 madarakani.

Hata hivyo mwaka 2015 rais Nguesso alilazimisha kufanyika kwa marekebisho ya katiba ambayo yaliondoa ukomo wa umri wa miaka 70 kipengele ambacho kingemzuia kuwania urais kwa mara nyingine mwaka uliofuata.

Marekebisho ya katiba pia yaliondoa kipengele cha mihula miwili ya miaka 7 madarakani na kuweka kipengele kipya cha mihula mitatu ya miaka 5 madarakani.

Uchaguzi wa mwaka 2016 ulifuatia vurugu za mara baada ya uchaguzi ambapo watu zaidi ya 17 waliripotiwa kufa, upinzani ukimtuhumu rais Nguesso ambaye alipata asilimia 67 ya kura zote kwa wizi, huku wapinzani wawili Jean-Marie Michel Mokoko na Andre Okombi Salissa, walikutwa na hatia ya makosa ya kuhatarisha usalama.

Ni akina nani wengine wanashindana na rais Nguesso kwenye uchaguzi huu?

Mwezi Januari mwaka huu, chama kikuu cha upinzani cha The Pan-African Union for Social Democracy (UPADS), kilitangaza kutoshiriki uchaguzi wa mwaka huu kwa kile ilichodai kuwa mazingira ya uchaguzi hayaridhishi na kupendekeza uchaguzi wa siku ya Jumapili, ufanyike mwaka 2023 na rais Nguesso asiwe mgombea.

Viongozi wengine wanaojaribu kumuondoa madarakani rais Nguesso ni pamoja na Guy Brice Parfait Kolelas, wa chama cha Union of Humanist Democratic.

Yumo pia Mathias Dzoni, waziri wa zamani wa fedha chini ya utawala wa Nguesso, ambapo katika uchaguzi wa mwaka 2016 alitangaza kutoshiriki akisema uchaguzi usingekuwa huru na haki.

Mwingine ni Albert Oniangue, ambaye ni mchungaji na aliwahi kutmikia jeshi la nchi hiyo hadi katika ngazi ya Kanali na amekuwa mgombea mpya katika siasa za nchi hiyo.

Wagombea wengine ni pamoja na Joseph Kignoumbi Kia Mbougou, Anguios Ngunguia Engambe na Dave Mafoula mwenye u,mri wa miaka 38 na mgombea kijana zaidi kwenye kinyanganyiro cha mwaka huu.

Hata hivyo, viongozi wa mashirika ya kiraia nchini humo wanasema kati ya wagombea wote 6 hakuna ambaye ana uwezo wa kumuondoa madarakani rais Nguesso.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.