Pata taarifa kuu
DRC-RWANDA-USALAMA

Jeshi la Rwanda lashtumiwa kuingia katika ardhi ya DRC

Mashirika ya kiraia mkoani Kivu kaskazini nchini DRC yanalaani kitendo cha wanajeshi wa Rwanda kuingia nchini humo na kutekeleza operesheni ya kuyasaka makundi ya waasi wa Rwanda katika eneo la Nyiragongo mbali kidogo na mji wa Goma.

Waasi wa kihutu wa Rwanda wa FDLR waendelea kuhatarisha usalama katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa DRC.
Waasi wa kihutu wa Rwanda wa FDLR waendelea kuhatarisha usalama katika baadhi ya maeneo ya mashariki mwa DRC. AFP PHOTO/ LIONEL HEALING
Matangazo ya kibiashara

Kwa Mujibu wa mashirika hayo ya kiraia eneo la Nyiragongo, hakuna anayeweza kukanusha hili, kwamba wanajeshi wa jeshi la Rwanda wamevuka mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kubaini kuongezeka kwa matukio yanayowasababshia wakaazi wa eneo hilo kuishi wakiwa na wasiwasi mkubwa, huku miongoni mwa matukio yaliyotajwa ni pamoja na mwanajeshi mmoja wa Rwanda kujeruhiwa kwa risasi katika eneo la Kabara, karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege wa Goma Ijumaa ya wiki iliyopita.

Mwenyekiti wa Mashirika hayo ya kiraia ya Nyiragongo Mambo Kawaya amewataka viongozi wa Jumuia ya nchi za Maziwa Makuu ICGLR kuingilia kati.

Juvenal Munubo Mubi, mbunge kutoka mkoa wa Kivu Kaskazini, amekiri kupokea ripoti kama hiyo ya wawakilishi kadhaa wa mashirika ya kiraia. Ametoa wito kwa wakuu wa nchi za maziwa makuu kukutana, kwa kuwa si mara ya kwanza jeshi la Rwanda kuivamia ardhi ya DRC.

Gavana wa mkoa wa Kivu Kaskazini hajatoa tamko lolote kuhusu hatua hii. Anatarajiwa kukutana na mjumbe wa DRC katika Jumuiya ya nchi za maziwa makuu (ICGLR) katika kitengo cha ufuatiliaji wa matukio maeneo ya mipaka ya nchi hizo Jumatano wiki hii.

Hivi karibuni, jukwaa linalofahamika kama Kivu Security Tracker, ikiwa ni kitengo cha shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch liliripoti kupitia mitandao ya kijamii mapigano kati ya jeshi la DRC na waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR katika eneo jirani na Rutshuru.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.