Pata taarifa kuu
MALAWI

Mahakama nchini Malawi, yabatilisha matokeo ya uchaguzi wa mwezi Mei 2019

Mahakama ya katiba nchini Malawi imebatilisha matokeo ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Mei 21 mwaka 2019.

Rais wa Malawi, Peter Mutharika akipungia katika moja ya ziara zake mwaka 2013, ushindi wake umetenguliwa na mahakama ya katiba
Rais wa Malawi, Peter Mutharika akipungia katika moja ya ziara zake mwaka 2013, ushindi wake umetenguliwa na mahakama ya katiba AFP/Amos Gumulira
Matangazo ya kibiashara

Majaji wa 5 wa mahakama hiyo kwa kauli wametoa hukumu inayofanana kubatilisha uchaguzi ambao ulimpa ushindi rais wa sasa Peter Mutharika.

Jaji kiongozi wa mahakama hiyo, Healey Potani, amesema uchaguzi uliofanyika mwezi Mei ulikuwa na dosari nyingi zilizoufanya uchaguzi huo usiwe huru, haki na wakuaminika.

Jaji Potani akitoa siku 150 kwa tume ya uchaguzi kuandaa uchaguzi mpya ambao utakuwa huru na kuaminika.

Punde baada ya uamuzi huu wafuasi wa chama kikuu cha upinzani cha MCP walikusanyika nje ya makao makuu ya chama chao wakiimba nyimbo za ushindi na kushangilia.

Mahakamani alikuwepo kinara wa upinzani Lazarus Chakwera na mwenzake wa chama cha UTM, Saulos Chilima ambao walifungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Katika uchaguzi huo tume ya uchaguzi ilimtangaza Peter Mutharika kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 38.6 ya kura zote.

Hata hivyo Chakwera ambaye alishika nafasi ya pili na Chilima aliyeshika nafasi ya tatu, walienda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo wakidai haukuwa huru.

Matokeo hayo kwa majuma kadhaa yalisababisha maandamano makubwa ya wafuasi wa upinzania huku Serikali ikilaumiwa pakubwa kwa kutumia nguvu kubwa kukabiliana na waandamanaji.

Chakwera anadai yeye ndiye alikuwa mshindi halali wa uchaguzi huo kwa kupata asilimia 35.4 ya kura zote.

Chilima ambaye alikuwa mshirika wa karibu wa rais Mutharika yeye alipata asiliamia 20.2 ya kura nae akidai uchaguzi haukuwa huru na uligubikwa na dosari nyingi, matamshi yaliyoungwa mkono na waangalizi wa kimataifa isipokuwa wale kutoka umoja wa Afrika.

Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo mengi ya nchi kufuatia uamuzi wa mahakama ya katiba ambayo imetaka kuundwa kwa chombo maalumu ambacho kitasimamia Serikali na kuandaa uchaguzi mkuu.

Licha ya upinzani kulalamikia matokeo ya uchaguzi huo, tume ya uchaguzi ilisisitiza kuwa ilifuata sheria katika kutangaza mshindi na kwamba hakukuwa na udanganyifu ambao ungefanya matokeo ya uchaguzi huo kuwa batili.

Tume ya haki za binadamu nchini Malawi imesema mwezi Octoba pekee wakati wa maandamano ya wafuasi wa upinzani, polisi na wanajeshi walitekeleza vitendo vya ukatili kwa kuwabaka wanawake hata mbele ya familia zao.

Wakizungumza nje ya mahakama ya katiba, Chakwera na Chilima wamewataka wafuasi wao kuheshimu uamuzi wa mahakama na kuwa watulivu wakati huu mchakato mpya wa uchaguzi ukiandaliwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.