Pata taarifa kuu
SOMALIA

Raia wa Somalia waendelea kusherehekea ushindi wa rais "Farmajo"

Raia wa Somalia kwa siku ya pili wanasherehekea ushindi wa Mohamed Abdullahi Mohamed anayefahamika kwa jina maarufu la "Farmajo" kuwa rais wao baada ya kuchaguliwa na wabunge siku ya Jumatano.

Wanasiasa wa Somalia wakisherehekea ushindi wa rais Mohamed Abdullahi Mohamed  mjini Mogadishu Februari 08 2017
Wanasiasa wa Somalia wakisherehekea ushindi wa rais Mohamed Abdullahi Mohamed mjini Mogadishu Februari 08 2017 Wikipedia
Matangazo ya kibiashara

Ushindi huu umeleta mwamko mpya na matumaini katika taifa hilo linaloendelea kukabiliwa na ukosefu wa usalama kwa sababu ya kundi la kigaidi la Al Shabab na maswala ya ufisadi.

Fadumo Dayib Mwanamke pekee aliyekuwa ameonesha nia ya kuwania urais na baadaye kujiondoa, amesema kuna matarajio makubwa kutoka kwa rais Farmajo na anachotakiwa kufanya ni kujihusisha na watu wema.

“Serikali hii mpya inastahili kuwa na Mawaziri wachache ambao watakuwa na uwezo wa kuwatumikia kikamilifu raia wa Somalia,” ameongeza hili kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Ushindi huu ulisababisha hata wanajeshi wa Somalia na maafisa wa polisi kusherehekea kwa kufwatua risasi hewani.

Wakaazi wa mji wa Mogadishu kwa muda mrefu, walikuwa hawajawahi kujitokeza katika barabara za mji huo lakini mambo yalikuwa tofauti siku ya Jumatano.

Aliyekuwa mgombea mwingine wa urais Ali Warsame, naye amesema Somalia imeamua kupiga hatua kwa kumpata rais Farmajo.

“Somalia iliamua kupiga hatua, tuna imani kuwa tumeonesha ukomavu wa kisiasa.Tunakaribisha mabadiliko, lakini kuna mengi ya kufanyia kazi,” amesema.

Mambo muhimu kumhusu rais Mohamed Abdullahi Mohamed:-

  • Umri wa miaka 54.
  • Anakuwa rais wa 9 wa Somalia.
  • Kati ya mwaka 2010-2011, alihudumu kama Waziri Mkuu kabla ya kujiuzulu.
  • Ni Mwanadiplomasia na Profesa wa maswala ya siasa na historia.
  • Ana uraia wa Somalia lakini pia wa Marekani.
  • Ajenda yake kuu ni kuhakikisha kuwa raia wa Somalia wanakuwa kitu kimoja, wanakuwa huru.
Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.