Pata taarifa kuu
BURUNDI

Tunataka uchunguzi ufanyike kuhusu vijana wa chama tawala nchini Burundi kupewa silaha na Serikali, wasema wanaharakati

Ikiwa ni miezi mwili imepita baada ya kuvuja kwa taarifa kutoka Umoja wa Mataifa nchini Burundi kuhusu uwepo wa shughuli za ugavi wa silaha kwa vijana wa chama tawala cha CNDD-FDD “Imbonerakure”, mashirika ya kiraia nchini humo yanataka taarifa hizo kuchunguzwa. 

Vijana wa chama tawala "Imbonerakure" wakiwa kwenye moja ya maonesho
Vijana wa chama tawala "Imbonerakure" wakiwa kwenye moja ya maonesho RFI
Matangazo ya kibiashara

Taarifa hii ilisababisha hata Serikali ya Burundi kumfukuza nchini humo aliyekuwa mkuu wa masuala ya usalama wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini humo na pia kukamatwa kwa mwanaharakati wa haki za binadamu na mtetezi wa haki za wafungwa Pieere Claver Mbonipa.

Muungano wa mashrika ya kiraia nchini humo umesaini waraka kwa rais wa Burundi Pierre Nkurunziza na kwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kufanyika kwa uchunguzi kuhusu taarifa hii.

Mratibu wa shughuli kwenye muungano wa mashirika ya kiraia Vital Nshimirimana amesema lengo hasa ni kutaka kujua ukweli kuhusu taarifa hii kwani serikali ya Burundi haitaki kufanyika kwa uchunguzi ili kutoa mwanga zaidi kuhusu taarifa za vijana wa chama tawala wanaopewa mafunzo ya kijeshi katika ardhi ya Congo.

Lengo hasa la waraka huu ni kuhakikisha mashirika haya yanakusanya saini za kutosha ndani ya majuma mawili kuishinikiza serikali na Jumuiya ya Kimataifa kuanzisha uchunguzi kuhusu taarifa hii ya kutatanisha.

Vijana wa Imbonerakure wa chama tawala nchini Burundi
Vijana wa Imbonerakure wa chama tawala nchini Burundi Desire Nimubona/IRIN/www.irinnews.org

Katika hatua nyingine Serikali ya Burundi imetupilia mbali pendekezo la Shirirka la raia nchini humo la kupiga kampeni ili kukusanya saini katika muda wa wiki mbili zijazo, kuilazimisha kuanzisha mchakato wa kuchunguza madai kwamba imegawa silaha kwa vijana wa chama tawala “Imbonerakure”.

Majibu ya Serikali ya Burundi hayakuwa na kigugumizi wakati Msemaji wa Serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba ametuhumu mashrika ya kiraia nchini humo kuendelea kuwa vibaraka wa vyama vya upinzani.

Umoja wa Mataifa tayari umeonya kuhusu kuendelea kushuhudiwa kwa mvutano wa kisiasa nchini humo pamoja na tuhuma kuwa chama tawala kimekuwa kikiwapa silaha vijana wake, hatua ambayo UN inaona huenda ikachochea vurugu nchini humo.

Haya yanajiri wakati huu ambapo nchi ya Burundi inajiandaa kufanya uchaguzi wake mkuu hapo mwakani, uchaguzi ambao unatarajiwa kumshuhudia rais Pierre Nkurunzinza akiwania nafasi hiyo chini ya mabadiliko ya sheria kwenye katiba ya sasa ambayo itamruhusu rais huyo kuwania tena urais.

Hata hivyo sheria hii ya mabadiliko ya katiba ilipingwa na wabunge.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.