Pata taarifa kuu
MALAWI

Wanaharakati nchini Malawi watoa siku 21 kwa serikali kutatua mzozo uliopo nchini humo

Wanaharakati nchini Malawi wamempa siku ishirini na moja rais wa nchi hiyo Bingu wa Mutharika kuhakikisha anatatua mgogoro uliopo nchini humo ama sivyo ategemee maandamano zaidi ya kumshinikiza kung'atuka madarakani.

Baadhi ya waandamanaji nchini Malawi
Baadhi ya waandamanaji nchini Malawi Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo nchini humo, Rafiq Hajat amesema kuwa wamemuandikia barua rais Mutahrika ya kumpa siku hadi tareh 16 mwezi wa 8 kuhakikisha anatoa majibu yanayoridhisha kwa wananchi wa taifa hilo kuhusiana na jinsi ya kutatua hali ngumu ya maisha nchini humo.

Hajat amesema kuwa endapo rais Mutharika hatotoa majibu mpaka kufikia tarehe 16 mwezi ujao, basi wataitisha maandamano makubwa siku inayofuata kushinikiza rais huyo kung'atuka madarakani na kuitisha uchaguzi mkuu.

Katika barua ambayo wameiandikia serikali, wanaharakati hao wanataka kuchunguzwa kwa mali za rais Mutharika pamoja na mawaziri wake wanaouunda serikali, kwakile wanaharakati hao walichodai ni ufujaji wa mali za nchi unaofanywa na viongozi hao.

Wanaharakati hao wameongeza kuwa hali ngumu ya uchumi iliyoikumba nchi hiyo imetokana na uzembe wa serikali kushindwa kutumia rasilimali za nchi kwa viongozi kujilimbikizia mali pamoja na kuvunja uhusiano wa kibalozi na nchi ambazo zinachangia nusu ya bejeti ya nchi hiyo wakitolea mfano taifa la Uingereza.

Rais Mutharika mwenyewe amewatuhumu viongozi wa upinzani nchini humo kwa kushiriki kuchochea vurugu ambazo mpaka sasa zimeshuhudia watu zaidi ya kumi na tisa wakipoteza maisha kutokana na maandamano yaliyoanza juma lililopita.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa viongozi ambao wanashiriki kuandaa maandamano hayo wamekimbilia msituni kujificha na kuonya hali hiyo huenda ikachochea vurugu zaidi nchini humo.

Tayari vyama vya kidini nchini humo vimelaani nguvu ambayo inatumiwa na vikosi vya serikali kutuliza machafuko hayo, huku pia wakimtuhumu rais Bingu wa Mutharika kwa jinsi anavyoongoza nchi hiyo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.