rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Togo Faure Gnassingbe

Imechapishwa • Imehaririwa

Serikali ya Togo yaagizwa kuandaa uchaguzi kabla ya mwisho wa mwaka

media
Maandamano ya kisiasa yaendelea kuathiri uchumi wa Togo. REUTERS/ ...

Mahakama ya Katiba nchini Togo, imeitaka serikali kuandaa Uchaguzi kabla ya mwisho wa mwaka huu. Tume ya Uchaguzi nchini humo CENI, imeagizwa kuhakikisha kuwa, inaweka mikakati ya kufanikisha Uchaguzi huo.


Uchaguzi ulitarajiwa kufanyika mwaka uliopita, lakini haukufanyika kwa sababu ya mzozo wa kisiasa ambao umeendelea kuwepo kwa karibu mwaka mmoja sasa, kushinikiza kuondoka madarakani kwa rais Faure Gnassingbe ambaye amekuwa akiongoza tangu mwaka 2005.

Mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Togo umesababisha mdororo wa kiuchumi, huku maduka yakiendelea kufungwa kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.

Raia wanaendelea kukabiliwa na hali mbaya ya kimaisha, huku mashirika mbalimbali yakiwataka wanasiasa, hasa serikali kutafutia ufumbuzi mgogoro huo.

Tangu mwezi Septemba, makumi ya maelfu ya watu mara kwa mara wamekua wakiingia mitaani kwa kuitikia wito wa muungano wa vyama 14 vya upinzani, wakitaka Rais Faure Gnassingbe ajiuzulu. Faure Gnassingbe alichaguliwa kwa muhula mwengine mnamo mwaka 2010 na 2015 katika uchaguzi uliozua utata na kususiwa na upinzani, baada ya kumrithi baba yake aliyetawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 38.