rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

Marekani Donald Trump

Imechapishwa • Imehaririwa

Matumizi ya shughuli za serikali yaidhinishwa Marekani

media
Rais wa Marekani Donald Trump apongeza hatua ya maseneta wa chama cha Democrats. REUTERS/Yuri Gripas

Mvutano kuhusu matumizi ya shughuli za serikali uliokua ukiendelea kwa siku tatu mfululizo nchini marekani, hatimaye umemalizika baada ya bunge la Seneti kupitisha matumizi ya muda kufadhili shughuli hizo.


Rais wa Marekani Donald Trump amekaribisha uamuzi huo kama ushindi mkubwa kwa upande wa kambi yake.

Baada ya mazungumzo mengi, viongozi wa chama cha Democrats katika baraza la Seneti walikubali muswada huo ambao utasaidia kufadhili huduma za serikali hadi februari 8, kwa lengo lililowekwa la kufikia mkataba kuhusu hatima ya mamia ya maelfu ya wahamiaji haramu waliowasili wakiwa vijana nchini Marekani, wanaojulikana kama "Dreamers".

Wawakilishi wa chama cha Democratic walisema kuwa wataunga mkono muswada huo kama utatoa hatma ya maelfu ya wahamiaji waliongia marekani wakiwa watoto ambapo sasa wanakabiliwa na kurudishwa sehemu walizotoka.

"Ninafurahi kusikia maseneta wa chama cha Democrats wameamua kuwa wenye busara," amesema Donald Trump katika taarifa fupi iliyosomwa na msemaji wake Sarah Sanders.

Hadi sasa wahamiaji hao wanalindwa na mpango wa kuwasadia watu walioingia Marekani wakiwa watoto DACA.

Matokeo ya moja kwa moja ya kumalizika kwa mvutano huo ni kuwa Rais Donald Trump atashiriki bila wasiwasi mwishoni mwa wiki katika mkutano kuhusu uchumi utakaofanyika Davos, Uswisi. Mwaka mmoja baada ya kuchukua hatamu ya uongozi, Rais Donald Trump atakuwa na fursa ya kutoa siku ya Ijumaa maono yake ya "Amerika kwanza" mbele ya viongozi wa nchi mbalimbali, viongozi wa makambuni na nyota tofauti kutoka duniani.