rfi

Hewani
  • RFI Kiswahili
  • Sikiliza taarifa ya Habari
  • RFI kwa Kifaransa

CAF CHAN Uganda Rwanda

Imechapishwa • Imehaririwa

Uganda Cranes kusaka ushindi wa kupeleka nyumbani dhidi ya Ivory Coast

media
Mchuano kati ya wenyeji Morocco na Sudan Januari 21 2018 www.cafonline.com

Timu ya taifa ya soka ya Uganda itashuka dimbani Jumatatu usiku kucheza na Ivory Coast katika mchuano wake wa mwisho wa kundi B, katika mashindano ya CHAN kwa wachezaji wanaocheza soka katika ligi za nyumbani barani Afrika.


Uganda Cranes inayofunzwa na Mfaransa S├ębastien Desabre, inaelekea katika mchuano huu wa mwisho, ikiwa na matumaini ya angalau kupata ushindi au kuondoka na alama moja katika michuano hii.

Vijana wa Desabre wamepata matokeo mabaya katika michuano ya mwaka huu, inayoendelea nchini Morocco baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza.

Uganda ilianza vibaya baada ya kufungwa na Zambia mabao 3-1 na kupoteza dhidi ya Namibia kwa bao 1-0 licha ya kutawala mchuano huo wiki iliyopita, mjini Marrakech.

Timu hii kutoka Afrika Mashariki, ilishiriki katika michuano hii mwaka 2011, 2014 , 2016 na sasa 2018 na katika kipindi hicho chote, imeondolewa katika hatua ya makundi.

Mchuano mwingine, wa kundi B ni kati ya Zambia na Namibia timu zote mbili ambazo zimefuzu katika hatua ya robo fainali.

Namibia ilianza vema kwa kuifunga Ivory Coast bao 1-0, ushindi ambao ilipata pia dhidi ya Uganda.

Mbali na kuishinda Uganda mabao 3-1, Chipolopolo iliishinda Ivory Coast mabao 2-0.

Mwishoni mwa wiki iliyopita katika michuano ya kundi A, wenyeji Morocco na Sudan walimaliza hatua ya makundi kwa kutofungana huku Guinea wakiondoka na alama tatu baada ya kuishinda Mauritania bao 1-0.

Siku ya Jumanne, itakuwa ni zamu ya kumaliza michuano ya kundi C.

Timu za Nigeria, Rwanda na mabingwa wa mwaka 2014 Libya, bado zina nafasi ya kufuzu katika hatua ya robo fainali.

Rwanda inahitaji sare kuwa katika nafasi nzuri ya kuendelea katika maashindano haya, itakapokutana na Libya.

Nigeria ambayo ina alama nne, nayo itamaliza mchuano wake dhidi ya Equiorial Guinea katika uwanja wa Ibn Batouta mjini Tangier.

Ratiba ya kundi la D:-

Tayari Congo Brazaville imefuzu katika hatua ya robo fainali baada ya kushinda mechi mbili za kundi hili, kuelekea mchuano wa mwisho dhidi ya Angola siku ya Jumatano.

Burkina Faso ambayo ina alama 1, ina nafasi ya kufuzu iwapo itaishinda Cameroon ambayo imeshaondolewa katika mashindano haya na kuomba kuwa Congo iifunge Angola.

Michuano ya robo fainali ni Jumamosi na Jumapili.