Pata taarifa kuu
CAF-SOKA-KLABU BINGWA-SHIRIKISHO

Vlabu vinavyofuzu hatua ya robo fainali vyaanza kufahamika

Michuano ya mwisho ya hatua ya makundi, kuwania taji la klabu bingwa na Shirikisho barani Afrika inamalizika mwishoni mwa wiki hii katika nchi mataifa mbalimbali barani Afrika.

Michuano ya klabu bingwa barani Afrika CAF
Michuano ya klabu bingwa barani Afrika CAF © CAF
Matangazo ya kibiashara

Klabu Bingwa

Baada ya Al-Merrikh na Al-Hilal za Sudan kuondolewa katika michuano hii kutokana na nchi yao kufungiwa na FIFA, Etoile du Sahel ya Tunisia, na Ferroviario Beira ya Msumbiji, zimefuzu katika hatua ya robo fainali kutoka kundi A.

Hatima ya kundi B, itafahamika siku ya Jumapili baada ya mchuano kati ya Zamalek ya Misri na Al-Ahli Tripoli ya Libya, lakini pia USM Alger ya Algeria dhidi ya CAPS United ya Zimbabwe.

USM Alger ina alama 8 sawa na Al-Ahli Tripoli. CAPS United ya Zimbabwe  ina alama sita huku Zamalek ikiwa na alama 5.

Kundi C, tayari Esperance de Tunis ya Tunisia na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambao ni mabingwa watetezi, wamefuzu katika hatua ya robo fainali. Saint George ya Ethiopia na AS Vita Club ya DRC zimeaga mashindano haya.

Mechi za kumaliza mechi za kundi hili zinchezwa Jumapili, Mamelodi Sundowns dhidi ya AS Vita Club jijini Pretoria lakini pia Esperance de Tunis dhidi ya Saint George mjini Rades.

Hatima ya kundi la D, itafahamika hivi leo baada ya mechi za mwisho, kuanzia saa nne usiku. Al-Ahly itamenyana na Coton Sport huku Wydad Casablanca dhidi ya Zanaco.

Zanaco ya Zambia wanaongoza kundi hili kwa alama 11, huku Wydad Casablanca ikiwa ya pili kwa alama tisa, huku Al-Ahly ikiwa na alama 8. Coton Sport imeshaondolewa.

Taji la Shirikisho

Klabu ya KCCA ya Uganda, iliteleza katika mchuano wake wa mwisho siku ya Ijumaa dhidi ya Club Africain Tunisia baada ya kufungwa mabao 4-0 katika mchuano wa  kundi A.

Matokeo haya, yameifanya KCCA kukosa nafasi ya kuingia katika hatua ya robo fainali licha ya kuanza vizuri michuano hii  kwa kushinda mechi 3 na kwa bahati mbaya kupoteza mechi tatu.

KCCA inayofunzwa na kocha Mike Mutebi imelazimika kuaga mashindano haya kwa alama 9 ikiwa katika nafasi ya tatu, huku FUS Rabat ya Morroco ikifanikiwa kufuzu ikiwa na alama tisa kwa sababu ina mabao 9 huku KCCA ikiwa na mabao 8.

Mbali na FUS Rabat, Club Africain imefuzu baada ya kumaliza ya kwanza kwa alama 12.

MC Alger ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia, zimefuzu kutoka kundi B. Mechi za kutamatisha kundi hili zinachezwa Jumamosi. CS Sfaxien dhidi ya MC Alger, Platinum Stars dhidi ya Mbabane Swallows.

ZESCO United ya Zambia tayari imefuzu kutoka kundi C, baada ya mchuano wake dhidi ya Al-Hilal ya Sudan kuondolewa katika michuano hii.

Kibarua kisalia  kati ya Smouha ya Misri na Recreativo do Libolo ya Angola, wanaocheza leo.

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ina kazi kubwa ya kuishinda Horoya ya Guinea siku ya Jumapili katika uwanja wa Kamalondo mjini  Lubumbashi, kujihakikishia nafasi ya kufuzu katika hatua ya robo fainali.

Mazembe ambao ni mabingwa watetezi, wanaongoza kundi hili la D kwa alama 9 sawa na Horoya ambao pia wanataka ushindi.

Supersport United ya Afrika Kusini, nayo ina nafasi ya kufuzu ikiwa itaishinda CF Mounana ya Gabon ambayo tayari imeondolewa katika michuano hii.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.