Pata taarifa kuu
CAF-HAYATOU-AHMED

Ahmed Ahmed amaliza utawala wa miaka 29 wa Issa Hayatou, CAF

Shirikisho la soka barani Afrika, Caf, hatimaye limepata rais mpya baada ya Ahmed Ahmed kuchaguliwa kwa kishindo na kumuangusha Issa Hayatou, moja ya viongozi wakongwe zaidi waliowahi kuhudumu kwa muda mrefu kwenye taasisi ya soka.

Rais mpya wa shirikisho la soka barani Afrika Caf, Ahmad Ahmad akizungumza mjini Addis Ababa baada ya ushindi wake. 16 Machi 2017.
Rais mpya wa shirikisho la soka barani Afrika Caf, Ahmad Ahmad akizungumza mjini Addis Ababa baada ya ushindi wake. 16 Machi 2017. REUTERS/Tiksa Negeri
Matangazo ya kibiashara

Ahmed amemshinda Hayatou kwa kura 34 kwa 20 katika uchaguzi ambao sasa unamaliza miaka 29 ya utawala wa Hayatou aliyekuwa akiongoza shirikisho hili la mpira barani Afrika toka mwaka 1988.

Ahmed, mwenye umri wa miaka 57 na baba wa watoto wawili, amekuwa kwa muda akifundisha soka na kucheza mpira kwa nyakati tofauti kabla ya kuchukua urais wa chama cha soka cha Madagascar mwaka 2003.

Uchaguzi wa mwaka huu umekuwa wa kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa Issa hayatou kupata upinzani mkali ukilinganisha na chaguzi nyingine zilizotangulia ambapo mara zote amekuwa akipitishwa kwa kishindo na wakati mwingine kukosa mpinzani.

Toka kutangaza kuwa atawania kiti cha urais kwenye uchaguzi wa mwaka huu, Ahmed alipata mara moja uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya viongozi wa mashirikisho ya soka barani Afrika, ambao walipenda sera za mgombea huyu aliyekuwa akijinasibu kufanya mabadiliko makubwa kwenye shirikisho hilo la kulibadili soka la Afrika.

Mwaka huu mara kadhaa imeshuhudiwa Issa Hayatou akiingia kwenye mvutano wa maneno na marais wa vyama vya soka toka nchi za kusini mwa Afrika COSAFA, ambao wao toka awali waliweka wazi msimamo wao kuhusu kumuunga mkono Ahmed Ahmed.

Na ni mwanzoni mwa juma hili tu baada ya kuanza kwa mkutano mkuu wa Caf, Issa Hayatou kupitia kamati ya utendaji waliridhia kwa kauli moja kuanza kusikiliza shauri la kinidhamu dhidi ya rais wa chama cha soka cha Zimbabwe, Phillip Chiyangwa, aliyeitisha mkutano wa marais toka nchi za COSAFA kujadili namna ya kumuondoa Issa Hayatou madarakani.

Uchaguzi wa mwaka huu pia umekuwa na mvuto wa aina yake, kwakuwa hata baadhi ya vyama vya soka ambavyo kwa miaka nenda rudi vimekuwa vikimuunga mkono Issa Hayatou kwenye chaguzi zilizopita, walibadili kibao na kutangaza hadharani kutomuunga mkono.

Kwanini Issa Hayatou ameshindwa?

Wachambuzi wa masuala ya soka wanasema kuwa kushindwa kwa Hayatou huenda kusitokane sana na sera zake kwa soka la Afrika, lakini kikubwa ni kutokana na ukweli kuwa amekaa madarakani kwa muda mrefu na wengi walianza kumuona kama mtawala wa kiimla kwenye shirikisho hili.

Kingine ambacho wachambuzi wa mambo wanaona kilimuangusha Issa Hayatou ni kutokana na ukaribu wake na aliyekuwa rais wa shirikisho la mpira duniani Fifa, Sepp Blatter ambaye anatumikia adhabu ya muda wa miaka 6 kutojihusisha na soka kutokana na ubadhilifu alioufanya wakati akiwa kiongozi.

Kwenye uchaguzi uliopita wa fifa, Issa Hayatou pia hakuonekana kumuunga mkono rais wa sasa Gianni Infantino, ambaye majuma mawili yaliyopita alifanya ziara kwenye nchi kadhaa za Afrika ambazo kwa sehemu kubwa zilimuunga mkono na kumpigia kura.

Kwanini Ahmed Ahmed ameshinda?

Ahmed Ahmed, mgombea ambaye awali alikuwa hapewi sana nafasi ya kumshinda Hayatou kwenye uchaguzi wa mwaka huu, alipata umaarufu na uungwaji mkono toka kwa baadhi ya viongozi wa soka baada ya kuonekana kuwa na ahadi muhimu ya kulibadili soka la Afrika.

Ahmed anayeoonekana kuwa mwanamabadiliko ndani ya Caf, ameahidi kufanyia marekebisho baadhi ya vifungu vya katiba ya Caf ambavyo kwa sasa vinampa madaraka makubwa rais.

Mbali na marekebisho ya katiba, Ahmed aliahidi kubadili baadhi ya mifumo ya uendeshaji wa mashindano makubwa barani humo, huku akiahidi kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwaajili ya maendeleo ya soka barani Afrika.

Licha ya kuanguka kwa Issa Hayatou kwenye nafasi yake, kiongozi huyu aliyeingia madarakani toka mwaka 1988, amefanya makubwa kwenye soka la Afrika, ikiwemo kupanua wigo wa mashindano ya Afrika na kupata makampuni makubwa yanayifadhili mashindano hayo.

Issa Hayatou pia amesaidia vyama vingi vya michezo barani Afrika kuwa na uwezo wa kujitegemea na pia kulifanya soka la Afrika kutambulika kimataifa ikiwa ni pamoja na kuliwezesha bara hilo kupata timu tano kwenda kwenye mashindano ya kombe la dunia.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.