Pata taarifa kuu
ALGERIA-WCQ 2018

Algeria yamfuta kazi Milovan Rajevac baada ya mechi 2

Shirikisho la soka nchini Algeria limetangaza kumfuta kazi, kocha mkuu wa timu ya taifa, Milovan Rajevac, baada ya kushindwa kuiongoza vema timu hiyo katika mechi za kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018.

Milovan Rajevac, aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Algeria, hapa kwenye mkutano wake na wanahabari mjini Algers, 14 JULAI 2016.
Milovan Rajevac, aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Algeria, hapa kwenye mkutano wake na wanahabari mjini Algers, 14 JULAI 2016. Farouk Batiche / AFP
Matangazo ya kibiashara

Rajevac anakuwa kocha wa pili kuwa muhanga wa kufutwa kazi na mwajiri wake, baada ya Algeria kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Cameroon kwenye mchezo wa raundi ya kwanza wa kusaka tiketi ya kwenda nchini Urusi.

Mserbia Rajevac ameiongoza timu hiyo katika mechi mbili pekee lakini alijikuta akikosolewa na baadhi ya wachezaji wa timu yake wakidai kuwa hawaridhishwi na mbinu za ufundishaji za kocha huyo.

Timu ya taifa ya Algeria ilikuwa inategemea kuchomoza na ushindi kwenye mchezo wake wa kundi B dhidi ya Cameroon, lakini mambo yakawaendea kombo na kujikuta wakilazimishwa sare ya bao 1-1.

Kabla ya kufutwa kazi, kocha Rajevac alikutana kwa mazungumzo na rais wa shirikisho la mpira la Algeria, Mohamed Raouraoua, ambapo baada ya mkutano wao, akatangaza kusitisha kandarasi ya kocha huyo.

Algeria ambayo mchezo unaofuata itacheza na timu ya taifa ya Nigeria, wakati huu imeshaanza mchakato wa kusaka kocha wa tatu katika kipindi cha mwaka mmoja, ambapo aliyekuwa kocha wake Christian Gourcuff aliacha kazi ya kuinoa timu hiyo mwezi April mwaka huu na kurejea kufundisha kwenye ligi kuu ya Ufaransa, League 1.

Rajevac mwenye umri wa miaka 62 hivi sasa, aliwahi kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Ghana, wakati timu hiyo ilipofanikiwa kuwa nchi pekee iliyofanikiwa kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la dunia mwaka 2010, iliyofanyika nchini Afrika Kusini.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.