Pata taarifa kuu
EURO 2016

Wales yafanya kweli, Uingereza wazomewa, Urusi yatolewa

Mechi za kundi B, michuano ya kombe la Ulaya zimepigwa siku ya Jumatatu na kushuhudia maajabu ya soka yakitendeka.

Mshambuliaji wa Wales, Gareth Bale akishangilia baada ya kuifungia timu yake goli.
Mshambuliaji wa Wales, Gareth Bale akishangilia baada ya kuifungia timu yake goli. REUTERS/Sergio Perez
Matangazo ya kibiashara

Wales waliokuwa na kibarua dhidi ya Urusi, walijikuta kibarua chao kinakuwa chepesi, baada ya kuchomoza na ushindi mnono dhidi ya Urusi.

Wales waliingia kwenye mechi hii wakiwa na lengo moja tu la kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Urusi, nia ambayo ilitimia baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Urusi iliyoonekana wazi kushindwa kuwamudu washambuliaji wa Wales.

Mchezaji wa Wales, Aaron Ramsey akikabiliana na mchezaji wa Urusi, wakati wa mchezo wao 20 juni 2016.
Mchezaji wa Wales, Aaron Ramsey akikabiliana na mchezaji wa Urusi, wakati wa mchezo wao 20 juni 2016. REUTERS/Vincent Kessler

Wales walipata bao la kwanza kupitia kwa Aaron Ramsey katika dakika ya 11 ya mchezo, bao ambalo ni wazi lilionekana kuwaduwaza Urusi ambao walijitahidi kuja juu lakini juhudi zao hazikufua dafu.

Wales walipata bao la pili katika dakika ya ishirini ya mchezo, ambapo mchezaji Neil Taylor aliiandikia timu yake bao la pili, lililodhihirisha nia ya wazi ya kikosi cha Coleman kuibuka na ushindi.

Dakika ya 67 ya mchezo mshambuliaji wa kimataifa wa Wales anayekipiga na klabu ya Real Madrid ya nchini Uhispania, Gareth Bale, alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Urusi na kumaliza mchezo.

Wales ilikuwa inahitaji ushindi dhidi ya Urusi, kujihakikishia nafasi ya kutinga kwenye hatua ya 16 bora, matokeo ambayo iliyapata na kuwafanya waongoze kundi B wakifuatiwa na Uingereza walioambulia sare kwenye mchezo wao dhidi ya Slovakia.

Kocha mkuu wa Wales, Chris Coleman, amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kiwango cha juu licha ya ugumu waliokuwa nao awali kuhusu namna Urusi ingecheza, ambapo ameongeza kuwa kiwango cha timuj yake nik bora zaidi hata kuliko ilivyokuwa kwenye mechi za kufuzu.

Kwa upande wake kocha mkuu wa Urusi, Leonid Slutski, amesema kuwa ataachia ngazi kukinoa kikosi hicho kwa kile alichosema kuwa ni muda wa kutoa nafasi kwa kocha mwingine kuichukua timu hiyo kuiandaa na michuano ya kombe la dunia itakayofanyika nchini mwaka mwaka 2018.

Kocha wa Urusi, Leonid Slutski.
Kocha wa Urusi, Leonid Slutski. REUTERS/Vincent Kessler

Leonid Slutski, amekiri timu yake kucheza chini ya kiwango kuliko alivyotarajia na kwamba haoni sababu ya kuendelea kukinoa kikosi hicho ikiwa wachezaji hawachezi kama alivyotoa maelekezo na itakuwa vigumu kwake kuiandaa kwa fainali za kombe la dunia.

Kwenye mchezo mwingine wa kundi B, Uingereza walikuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Slovakia, kwenye mchezo ambao ulishuhudia timu hizi zikitoka sare ya bila kufungana.

Kikosi cha Uingereza ambacho kilianza kipindi cha kwanza bila ya nahodha wake wa kila siku Wayne Rooney, kilikosa mbinu kabisa ya kiwaadhibu Slovakia.

Kocha wa Uingereza, Roy Hodgson akiwa na wachezaji wake wakitoka baada ya mechi yao na Slovakia, 20 juni 2016.
Kocha wa Uingereza, Roy Hodgson akiwa na wachezaji wake wakitoka baada ya mechi yao na Slovakia, 20 juni 2016. REUTERS/Max Rossi

Licha ya kosakosa kadhaa za wachezaji Daniel Sturridge na Jarmie Vardy, hazikutosha kusababisha madhara kwenye lango la Slovakia ambayo ukuta wake ulikuwa mgumu kupitika kwa dakika zote 90.

Kwa matokeo haya, yameendelea kumuweka pabaya kocha wa Uingereza Roy Hodgson anayekosolewa pakubwa kutokana na kikosi chake kukosa makali hali iliyosababisha kushindwa kupata matokeo ya kuisaidia timu hiyo kuingia kwa kishindo kwenye hatua ya 16 bora.

Akizungumza mara baada ya mchezo, kocha huyo amekiri wachezaji wake kukosa umakini wakati wa kumalizia mipira ambayo ingeweza kuwa magoli na kuwapa ushindi, na kudai kuwa kikubwa alichokuwa anakitaka kama kocha ni kuingia kwenye hatua ya mtoano.

Hodgson ameongeza kuwa anafahamu mashabiki hawakufurahishwa na kiwangok kilichooneshwa na timu yake, ambapo wakati mpira ukielekea ukingoni, mashabiki walimzomea pamoja na wachezaji wake kwa kushindwa kuchomoza na ushindi kwenye mechik muhimu.

Wachezaji wa Slovakia na benchi la ufundi wakishangilia baada ya kumalizika kwa mchezo wao na Uingereza.
Wachezaji wa Slovakia na benchi la ufundi wakishangilia baada ya kumalizika kwa mchezo wao na Uingereza. REUTERS/Robert Pratta Livepic

Kwa matokeo haya, Wales wanaongoza kwenye kundi B wakiwa na alama 6, mbele ya Uingereza yenye alama 5, huku Slovakia yenyewe ikimaliza kwenye nafasi ya tatu ikiwa na alama 4, na hivyo kusubiri ikiwa itakuwa miongoni mwa timu 4 zitakazopewa nafasi ya kuingia hatua ya 16 bora.

Sheria mpya ya mashindano ya mwaka huu, inatoa nafasi kwa timu nne zilizomaliza kwenye nafasi ya tatu zikiwa na matokeo mazuri.

Moja ya kanuni zitakazotumika kutambua timu hizo ni pamoja na ulinganifu wa mabao ya kufunga na kufungwa, idadi ya alama ilizomaliza nazo, nidhamu kwa timu husika pamoja na viwango vya timu bora kwenye orodha ya Uefa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.