Pata taarifa kuu
EUROPA

Mabingwa wa Europa Atletico Madrid waondolewa huku Newcastle United, Tottenham na Chelsea wakifuzu

Mabingwa Watetezi wa Kombe la Europa Atletico Madrid wameondoshwa kwenye mashindano hayo licha ya kupata ushindi wa goli 1-0 dhidi ya wachezaji kumi wa Timu ya Rubin Kazan. Atletico Madrid wameondoshwa kwa jumla ya magoli 2-1 baada ya kufungwa katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Uhispania kwa magoli 2-0 lakini jana walishindwa kuonesha cheche zao.

Mshambuliaji wa Atletico Madrid Radamel Falcao akihuzunika baada ya timu yake kuondolewa kwenye Europa
Mshambuliaji wa Atletico Madrid Radamel Falcao akihuzunika baada ya timu yake kuondolewa kwenye Europa
Matangazo ya kibiashara

Mshambuliaji Radamel Falcao alifunga goli lake la mwisho kwenye mashindano ya Kombe la Europa na hivyo Mabingwa Watetezi kushindwa kutinga hatua ya 16 bora huku Rubin Kazan ikishuhudia mchezaji wake Gonzalez Cesar akilimwa kadi nyekundu.

Vijogoo vya Jiji Liverpool licha ya kupata ushindi wa magoli 3-1 mbele ya Zenit St Petersburg wameondoshwa kwenye mashindano ya Europa kutokana na wageni wao kunufaika na ushindi wa magoli 2-0 walioupata nyumbani.

Zenit St Petersburg ilikuwa ya kwanza kufunga goli kupitia Mshambuliaji wake Givanildo Vieira de Souza maarufu kama Hulk akitumia makosa ya beki Jamie Carragher kabla ya Luis Suarez hajasawazisha kupitia mpira wa adhabu ndogo.

Joe Allen alifunga goli la pili kabla ya mapumziko na baadaye Suarez akakwamisha goli la tatu kwa Liverpool lakini halikutosha kuwavusha kutinga hatua ya kumi na sita bora kwenye mchuano wa Europa.

Mabingwa wa Zamani wa Kombe la Mabingwa Barani Ulaya Chelsea nao walifuzu baada ya kutoka sare ya goli 1-1 mbele ya Sparta Prague huku wakinufaika na ushindi walioupata kwenye mchezo wa kwanza.

Eden Hazard ndiyo aliisaidia Chelsea kusonga mbele baada ya Sparta Prague kufunga goli la mapema kupitia David Lafata ambalo liliwaweka kwenye wakati mgumu The Blues lakini walirejesha matumaini baada ya kupata goli la dakika za lala salama.

Tottenham Hotspurs imefuzu katika hatua ya kumi na sita bora baada ya kupata sare ya goli 1-1 mbele ya Olympique Lyon mchezo ambao ulitawaliwa na ubabe pamoja na ghasia za nje ya uwanja.

Lyon walikuwa wa kwanza kufunga goli kupitia kwa Maxime Gonalons kabla ya Mousa Dembele kusawazisha na kukata tiketi ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo ya Europa wakipata faida kutokana na ushindi wa nyumbani wa magoli 2-1.

Newcastle United nao wamefanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya Europa baada ya kupata ushindi mwembamba wa ugenini dhidi ya Metalist Kharkiv kwa goli 1-0.

Shola Ameobi ndiye alifunga goli la ushindi kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa Moussa Sissoko huku mshambuliaji Papiss Cisse akikosa nafasi nyingi za wazi kwenye mchezo huo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.