Pata taarifa kuu
MAREKANI-SYRIA-USALAMA

Trump: Nitatumia nguvu kujibu shambulio la kemikali Syria

Rais wa Marekani Donald Trump, katika mkutano na waandishi wa habari, ameapa " kutumia nguvu " kujibu madai ya shambulio la kemikali linaodaiwa kutekelezwa katika mji wa Douma na majeshi ya Syria siku ya Jumamosi.

Rais wa Marekani ameionya Syria, akisema kuwa "watatumia nguvu" kujibu madai ya shambulio la kemikali nchini Syria.
Rais wa Marekani ameionya Syria, akisema kuwa "watatumia nguvu" kujibu madai ya shambulio la kemikali nchini Syria. REUTERS/Yuri Gripas
Matangazo ya kibiashara

Kauli hii ya rais wa Marekani inakuja wakati ambapo mataifa kadhaa ya magharibi yakisema kuwa bado yanatafakari hatua watakayoichukua.

Mashahidi wanasema watu wengi waliuawa katika shambulio hilo, lakini idadi kamili haijathibitishwa.

Makadirio ya idadi ya watu waliouawa katika shambulio linaloshukiwa kuwa la kemikali ni kuanzia watu 42 hadi zaidi 60, lakini makundi ya kitabibu yanasema idadi hiyo inaweza kuongezeka baada ya wahudumu wa uokoaji kuweza kufika kwenye sehemu za chini za majengo ambako mamia ya familia walikuwa wamekimbilia kuepuka mashambulio ya mabomu.

Shambulio hili limeendelea kuzua sintofahamu kati ya nchi zenye nguvu duniani, ambazo kwa sasa zimegawanyika kuhusu vita vinavyoendelea nchini Syria.

Urusi imeendelea kuunga mkono utawala wa Bashar Al Assad na kushirikiana na majeshi ya Syria kwa kuendesha mashambulizi ya hapa na pale dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi katika Ghouta ya mashariki.

Bw Trump amesema kuwa hatua ya kujibu shambulio hilo itaamuliwa katika kipindi cha "muda mfupi".

“Tuna njia nyingi za kijeshi, hatutashindwa kujibu, “ rais wa Marekani amesema katika mkutano na waandishi wa habari.

Shambulio hilo limezua mvutano katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya Marekani na Urusi.

Balozi wa Urusi katika baraza hilo Vassily Nebenzia, amesema shambulio hilo lilipangwa na kuionya Marekani kutothubutu kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria, akibaini kwamba hatua hiyo inaweza kuzua sintofahamu.

Kauli hiyo ya Urusi imepingwa vikali na Balozi wa Marekani kwenye Baraza la Uslama la Umoja wa Mataifa Nikki Haley, ambaye amesema kuwa wanaounga mkono jeshi la Syria, wana "damu ya watoto wa Syria " mikononi mwao.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.